Habari

Tamaa ya wakurugenzi wa KTDA ilivyoharibu bei ya chai

Na PETER MBURU December 11th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

BAADHI ya wakurugenzi wa Shirika la Ustawi wa Chai nchini (KTDA) walihusika katika kusambaza chai duni kwenye mnada wa Mombasa ili kunufaika na bei iliyowekwa na serikali.

Hii ni kulingana na ufichuzi wa Bodi ya Chai ya Kenya (TBK).

Ukaguzi wa kina uliofanywa na Bodi ya Chai ya Kenya (TBK) umefichua mtandao mpana wa ukiukaji wa viwango vya uzalishaji wa chai, uliohusisha baadhi ya wakurugenzi wa KTDA, mameneja wa viwanda, na maafisa wengine waliotajwa kunufaika kwa kupotosha mfumo wa mauzo ya chai.

Kwa mujibu wa TBK, maafisa hao walielekeza baadhi ya viwanda, hasa vile vya upande wa Magharibi mwa Bonde la Ufa, kupokea na kusambaza chai ya ubora hafifu katika mnada wa Mombasa.

Hatua hiyo ilifanyika baada ya serikali kuanzisha bei ya chini ya takribani Sh314 kwa kila kilo ya chai mnamo Julai 2021, ili kuhakikisha wakulima wa mashamba madogo hawaathiriwi na bei ya chini kupita kiasi. TBK inasema baadhi ya wakurugenzi waligeuza hatua hiyo kuwa mwanya wa ulaghai kwa kuhimiza majani mabichi duni kwa sababu walijua bei ya chini ingetolewa bila kujali ubora wa chai.
Kwa mujibu wa Bodi ya Chai, ukaguzi katika maeneo mbalimbali ulibaini kuwa kiwango cha ubora wa majani kilikuwa kimeshuka hadi chini ya asilimia 50, kinyume cha kiwango cha chini kinachokubalika cha asilimia 60. Kushuka huku kwa ubora kulitokana na wakulima kuzoea kuvuna majani duni kwa sababu walikuwa na uhakika wa bei.

Hali hii ilisababisha mrundikano wa chai isiyouzwa katika maghala ya KTDA, huku akiba ikipanda hadi kilo milioni 104 mwaka 2024 ikilinganishwa na milioni 37 tu mwaka 2021. Kutokana na chai kutouzwa, KTDA ilisema  ililazimika kukopa Sh12.8 bilioni ili kuwalipa wakulima. Tatizo la  ubora duni lilikumba wakulima wa Kericho, Bomet, Nyamira, Kisii, Nandi, Vihiga na Trans Nzoia. Wanachama wa Kamati ya Kilimo ya Bunge la Taifa waliwalaumu baadhi ya wakurugenzi wa KTDA kwa kunufaika na zabuni za viwanda, na wakataka uchunguzi ufanywe kuhusu mtindo  wa maisha ya maafisa hao.

Ripoti ya bunge ilionyesha pia kuwepo kwa udanganyifu wa mizani ambapo wakulima walipewa uzito mdogo kuliko wa chai waliyowasilisha, jambo lililopunguza mapato yao.

Wakulima walilalamika mbele ya kamati kuwa ufisadi, matumizi mabaya ya fedha na gharama za juu za uzalishaji zimewafanya wapate mapato duni kuliko wenzao wa eneo la Mlima Kenya.

KTDA inahudumia takriban wakulima wadogo 600,000 nchini, wengi wao wakiwa katika maeneo yaliyoathirika.

Katika ukaguzi mwingine, TBK ilibaini kuwa viwanda vya KTDA vilikuwa na madeni ya Sh26 bilioni kufikia Juni, ikitaja ukosefu wa nidhamu katika mikopo.

Hata hivyo, KTDA ilijitetea ikisema ilibidi ikope ili kuwalipa wakulima, baada ya chai isiyouzwa kufikia kilo milioni 104

 Wakulima kutoka maeneo hayo waliwasilisha malalamishi rasmi mbele ya kamati, wakidai kuwa vitendo vya wakurugenzi, mameneja na makarani vimesababisha kupungua kwa bei ya chai yao katika mnada, ikilinganishwa na wakulima wenzao wa eneo la Mlima Kenya.

Walitaka mageuzi ya haraka katika usimamizi wa KTDA na uchunguzi wa kina wa wanaoshukiwa kuhusika.