Tineja apigwa na umeme na kufa kwenye disko matanga Oyugis
MVULANA ni kati ya watu wawili ambao waliaga dunia baada ya kupigwa na umeme kwenye disco matanga mnamo Jumamosi Kaunti ya Homa Bay.
Tineja huyo Antipus Odongo na mtu mwingine walikufa mjini Oyugis, Rachuonyo Kusini. Walifariki kutokana na hitilafu ya umeme mahali walipokuwa wakisakata densi saa nane usiku wa kuamkia Jumamosi.
Waliokwepo kwenye disko matanga hiyo walisema tukio hilo lilijiri wakati ambapo mvua ilikuwa ikinyesha. Naibu Chifu wa Lokesheni ya Oyugis Magharibi Warren Omollo alisema wawili hao waliaga dunia papo hapo.
Bw Omollo alisema disco matanga hiyo ilifanyika mtaa wa Ragama viungani mwa mji wa Oyugis.
“Kuna wale ambao walikuwa wakisakata densi uwanjani wakati wa tukio hilo. Wale ambao walikuwa ndani ya jengo ambako hafla hiyo iliandaliwa hawakuathirika,” akasema Bw Omollo
Uchunguzi wa awali umebaini hitilafu hiyo ilitokea wakati ambapo nyaya za jenereta ambayo ilikuwa ikisambaza umeme, zilikumbwa na hitilafu.
“Mtu mwengine alijeruhiwa wakati wa tukio hilo. Alikimbizwa hospitalini kupokea huduma za kimatibabu,” akaongeza afisa huyo wa utawala.
Kamanda wa Polisi wa Rachuonyo Kusini Philemon Saera alithibitisha tukio hilo na kusema uchunguzi bado unaendelea.
“Tumemwaagiza meneja wa klabu, mmiliki wa disko na aliyewaalika klabuni waje kituoni. Watahojiwa,” akasema Bw Saera.