Tokeni nyumbani mtafute kazi kwa miradi ya serikali, Ruto aambia Wapwani

RAIS William Ruto amewataka vijana wa Pwani kujituma na kujitokeza kutoka manyumbani mwao ili kusaka kazi katika miradi ya serikali inayolenga kutoa nafasi za ajira kwao.
Akizungumza wakati wa kuweka jiwe la msingi katika nyumba za bei nafuu za Tezo Kaunti ya Kilifi, Rais Ruto alisema kuwa serikali ilikuwa imetoa nafasi za ajira ila haingewafuatilia vijana ili iwakabidhi kazi hizo.
“Huku taifa likiendelea kusonga mbele, tunapaswa kuhakikisha kuwa Kilifi imeendelea. Nataka kuwaambia kuwa tumepanga nafasi za ajira kupitia mpango kama huu wa nyumba za bei nafuu, ila ajira haitakuja kubisha mlangoni. Munapaswa kutoka nyumbani kwenyu na mtafute hizi kazi,” akasema.
Rasi Ruto, aliwataka vijana hao kujitokeza na kuulizia nafasi hizo za ajira katika miradi hiyo ya serikali na miradi mingine ya serikali yake.
Kwa mujibu wake, nafasi hizo zilikuwepo katika Nyumba za bei nafuu zinazojengwa sehemu mbalimbali mbali eneo hilo. Hii ni ikiwemo Nyumba 1000 huko Tezo, 1500 Mtwapa, 1000 Malindi, 500 eneo la Watamu, 500 huko Bofa na 500 mjini Kilifi.
Rais Ruto ambaye alieleza nia ya serikali yake kutengeneza nafasi nyingi za ajira katika eneo hilo na nchini kote, alisema kuwa serikali ililenga kutumia Bahari Hindi kama chanzo cha maendeleo ya kiuchumi.

“Tunajenga sehemu ya samaki kutua itakayogharimu Sh250 milioni na kufikia Septemba itakuwa imekamilika. Baada ya hapo tutatoa boti 125 za uvuvi kuhakikisha kuwa vijana wetu wanaweza kuenda kuvua hata kwa siku kumi na kuleta samaki tutakazo chakata. Fanyeni kazi na MCA na wabunge wenyu ili tusonge mbele pamoja,” akasema Rais Ruto.
Rais Ruto aliyekuwa katika siku yake ya nne katika ukanda wa Pwani, aliahidi wakazi kuwa angemaliza suala la uskwota kufikia mwisho wa 2025. Alieleza kuwa serikali yake ilikuwa imetenga fedha za kununua ardhi zinazomilikiwa na mabwanyenye wasiokuwepo ili kuwapa makazi wenyeji.
Licha ya kukosolewa, Rais Ruto aliitetea serikali yake ya mseto, inayojumuisha viongozi wa upinzani, kwa wakazi wa Tezo, akihakikisha kuwa ililenga kuboresha maisha ya Wakenya.
Aidha, alisema kuwa alikuwa ameungana na kiongozi wa ODM Raila Odinga kwa niaba ya taifa la Kenya.
Rais Ruto aliahidi kukamilisha miradi katika chuo kikuu cha Pwani ikiwemo kujenga bweni la wanafunzi 1000, hospitali na shule katika eneo la Tezo, na kujenga barabara la Chuo Kikuu cha Pwani kuelekea Ganze.
Alikuwa ameandamana na Naibu wa Rais Kithure Kindiki, Spika wa Seneti Amason Kingi, Waziri wa Madini Hassan Joho, Waziri wa Michezo Salim Mvurya, Waziri wa Ardhi na Nyumba Alice Wahome, gavana wa Kilifi Gideon Mung’aro, mbunge wa eneo hilo Owen Baya na Amina Mnyazi wa Malindi miongoni mwa wengine.