Habari

Tuko tayari kujinyima na kuteua mtu mmoja kuangusha Ruto – Viongozi

Na KEVIN CHERUIYOT, CHARLES WASONGA February 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

VIONGOZI wa upinzani walitumia hafla ya uzinduzi wa chama Peoples’ Liberation Party (PLP) kuweka wazi mpango wao wa kubuni muungano mpya utakaomwondoa mamlakani Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2027.

Wakiongozwa na kinara wa chama hicho (zamani Narc-Kenya), Martha Karua na mwenzake wa Wiper Kalonzo Musyoka, azimio la wanasiasa hao lilikuwa moja; kuuondoa mamlakani utawala wa Kenya Kwanza katika uchaguzi mkuu ujao.

Bi Karua alisema japo angependa kuwa mgombeaji wa urais wa muungano huo mpya, yu tayari kumuunga mkono mgombeaji mwingine yeyote ambaye huenda akabainika kuwa bora zaidi.

Wao ni pamoja na Bw Musyoka, aliyekuwa naibu wa rais Rigathi Gachagua, kiongozi wa chama cha Democratic Action Party (DAP-K) Eugene Wamalwa, aliyekuwa Waziri wa Usalama, Dkt Fred Matiang’i wa chama cha United Progressive Alliance (UPA), Morara Kebaso wa chama cha Injection of National Justice, Economic and Civic Transformation, (INJECT), Jimi Wanjigi wa Safina miongoni mwa wengine.

Bi Karua alisema kuwa umoja ndio utakuwa msingi wa muungano ambao utajengwa kusudi wafanikishe ajenda yao ya kumwondoa mamlakani Rais Ruto na washirika wake wote.

“Nimeelezea nia yangu ya kuwania urais sawa na kaka zangu, Kalonzo Musyoka na Rigathi Gachagua. Hata ndugu yetu mdogo Morara Kebaso na wengine hapa pia wana ndoto hiyo hiyo huku wengine wakitarajiwa kutangaza azma yao baadaye. Lakini muhimu ni kwamba sharti kila mmoja wetu aweke mbele maslahi ya taifa kuliko ya kibinafsi. Kwa hivyo, yeyote atakayeteuliwa, kwa njia ya uwazi, sote tutapiga foleni nyuma yake,” Bi Karua akaeleza.

Kuanzia mwaka jana, Bw Musyoka, amekuwa akikariri kuwa atawania urais katika uchaguzi mkuu ujao na kuwataka viongozi wengine kumuunga mkono.

“Baada ya kuunga mkono Raila Odinga mara tatu katika chaguzi za 2013, 2017 na 2022, sasa ni zamu yake na viongozi wengine wa Azimio kuniunga mkono. Mimi ndiye ninayefaa zaidi kumwondoa Rais Ruto mamlakani 2027 na anafahamu hilo ndiyo maana juzi alisema akiwa Homa Bay kwamba yuko tayari kupambana nami,” Bw Kalonzo alisema Novemba 18.

Alikuwa akimjibu Rais Ruto, ambaye akiwa ziarani katika eneobunge la Suba Kaskazini alipuuzilia mbali azma ya urais ya Bw Musyoka akisema; “Nitamshinda mapema zaidi.”

Naye Bw Gachagua, mnamo Jumatano alielezea nia yake ya kuwania urais mwaka wa 2027 licha ya kwamba sheria inamzuia mtu aliyetimuliwa mamlakani kwa ukiukaji wa katiba kushikilia wadhifa wa kuchaguliwa au kuteuliwa.

Kwenye mahojiano katika redio zinazopeperusha matangazo kwa lugha ya Kikamba, Bw Gachagua alieleza kuwa kesi aliyowasilisha mahakamani kupinga kutimuliwa kwake afisini, imempa afueni kisiasa kwani anaweza kuwania urais mradi kesi hiyo haijaamuliwa.

Alitaja kesi zilizomkabiliwa Dkt Ruto na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) ambazo alisema hazikuwazuia kuwania katika uchaguzi mkuu wa 2013.

Jana, Bw Gachagua na Musyoka pia walikariri haja ya wao kubuni muungano thabiti na wenye nguvu ili “kuleta ukombozi wa tatu nchini Kenya”.

“Tutaungana liwe liwalo kuiondoa Kenya Kwanza mamlakani ili watoto wetu wapate elimu nzuri, sekta yetu ya afya iweze kufanya kazi, wafanyakazi wasibebeshwe mzigo mzito wa ushuru na wa nyumba ambao unafaidi watu wachache na rafiki wa wale walioko mamlakani,” Bw Gachagua akaeleza.

Akiikemea serikali ya Rais Ruto, naibu wa rais wa zamani alisema, “Sijawahi kuiona serikali ya matapeli kama vile Kenya Kwanza. Tutawaambia Wakenya siri tunazozijua kuhusu Bw Ruto.”

“Raila tungependa kukupa ushauri; achana na mtu huyo.”

Mbunge huyo wa zamani wa Mathira aliwaonya wenzake kwamba wajihadhari na Rais Ruto ambaye alimtaja kama “mwanasiasa mjanja anayeweza kuvuruga ajenda yetu ya kukomboa taifa hili”.

Naye Bw Musyoka akasema: “Muungano wetu utakuwa ni ule wa vitendo. Wale wanaodhani kwamba tutasambaratika wanaota ndoto ya mchana.”

Bw Wanjigi naye alisema, “Lazima tushirikiane kwa umoja kuondoa matatizo yanayokumba nchi hii. Martha (Karua), lazima tuungane kuboresha maisha ya Wakenya baada ya kumshinda Ruto.”