Habari

Tulieni! Ida, wadhamini waingilia kati kutuliza joto ODM

Na Collins Omulo January 7th, 2026 Kusoma ni dakika: 3

IMEBIDI Bodi ya Wadhamini wa ODM iingilie kati kuokoa chama hicho chenye umri wa miaka 20 kisije kikasambaratika.

Hatua hiyo ilichochewa na hofu kuwa mvutano wa sasa unaweza kukivunja chama miezi mitatu tu baada ya kifo cha kiongozi wake wa muda mrefu, Raila Odinga.

Hatua hiyo pia imempa muda zaidi Seneta wa Nairobi na Katibu Mkuu wa ODM, Edwin Sifuna, ambaye anakabiliwa na hatari ya kufukuzwa kutoka chamani.

Wadhamini hao, walioteuliwa na marehemu Raila Odinga, wana jukumu la kuhakikisha uthabiti na usimamizi wa jumla wa chama, hasa wakati wa mabadiliko ya uongozi kama yale yanayokikumba chama kwa sasa.

Kabla ya bodi kuchukua hatua, Bw Sifuna alikuwa akishinikizwa na baadhi ya wanachama ajiuzulu.

Walimshutumu kwa kushirikiana na “maadui” wa chama, wakisema kitendo hicho ni sawa na usaliti na kinastahili adhabu ya kufukuzwa.

Kwa upande wake, Bw Sifuna, ambaye pia ni msemaji wa ODM, alidai baadhi ya wanachama wanaongozwa na maslahi binafsi na wanajaribu “kuuza” ODM kwa jina la kuunga mkono azma ya Rais William Ruto ya kuwania muhula wa pili. Alisisitiza kuwa Raila Odinga hakuwahi kusema ODM ingeunga mkono azma hiyo.

Hata hivyo, mkutano wa ngazi ya juu uliohusisha watu wenye ushawishi mkubwa ndani na nje ya chama, akiwemo mjane wa marehemu Waziri Mkuu, Bi Ida Odinga, ulizima msukumo wa kumfukuza Seneta Sifuna.

Chanzo cha karibu kilisema kuwa juhudi hizo hazikuwa na baraka za vigogo wa chama.

Vyanzo kadhaa vilivyozungumza na Taifa Dijitali vilifichua kuwa hatua ya Seneta wa Migori, Eddy Oketch, ya kutaka Seneta Sifuna avuliwe nyadhifa zake zote za bungeni na kufukuzwa ODM iliwashangaza maafisa wakuu wa chama.

Bodi ya Wadhamini imepanga mkutano na wahusika wote muhimu ili kushughulikia suala hilo.

Miongoni mwa wanaotarajiwa kushiriki mkutano huo ni Kiongozi wa ODM na Seneta wa Siaya, Dkt Oburu Oginga; Mweka Hazina wa Kitaifa Timothy Bosire; Mwanasheria Mkuu wa zamani na aliyekuwa Seneta wa Busia, Amos Wako; Naibu Katibu Mkuu Agnes Zani; na Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa chama, Joshua Kawino.

Watu wa ndani ya chama pia walihofia kuwa ombi hilo, lililowasilishwa bila mashauriano ya kina, lingeweza kusababisha mpasuko mkubwa ndani ya ODM na kudhoofisha uwezo wake wa kujadiliana kisiasa kuelekea uchaguzi wa 2027.

“Hofu kubwa ndani ya uongozi wa juu wa chama ni kuwa mchakato ulioanzishwa na Seneta Eddy ungewanufaisha wale wanaojua kuwa ODM iliyo imara na yenye umoja itaingia mezani kwa mazungumzo ikiwa na nguvu zaidi,” kilisema chanzo kimoja kwa siri.

Pia kulikuwa na wasiwasi wa kukera ngome ya kura ya Magharibi mwa Kenya, ambayo ni eneo muhimu kwa ODM, iwapo “mwana wao” Sifuna angefukuzwa au kuvuliwa wadhifa.

“Haiwezekani Magharibi mwa Kenya ikubali kimya kimya kuona Sifuna akifukuzwa katika chama ambacho wamekiunga mkono tangu uchaguzi wa 2007,” kilisema chanzo kingine.

Kudumisha falsafa ya “kusanya wote, usiwatawanye” ya marehemu Raila Odinga pia kulitajwa kuwa sababu mojawapo ya kuondolewa kwa ombi la kutimua Sifuna.

Vyanzo vilifichua kuwa ilikubaliwa barua ya Seneta Oketch iwekwe kando hadi mkutano wa viongozi wakuu wa ODM na Wadhamini ufanyike, kwa lengo la kujenga umoja ndani ya chama ambacho kimekuwa kikikumbwa na migogoro ya ndani tangu kifo cha Raila Odinga Oktoba mwaka jana.

“Mkutano huo pia utachunguza uwezekano wa kusuluhisha mzozo kati ya Junet Mohamed na Seneta Sifuna, ambao wamekuwa wakitupiana lawama kuhusu watu wanaodaiwa kutaka kuuza ODM,” kilisema chanzo kingine.

Msimamo na lugha ya barua ya Seneta Oketch ya kuondoa ombi lake la awali ilionyesha wazi kuwa kulikuwa na mkutano wa ngazi ya juu uliomfanya abadilishe msimamo haraka.

Katika barua Jumanne iliyoandikwa na wakili wake Gad Aguko, Seneta Oketch alisema mabadiliko hayo yalitokana na “mashauriano mapana” na Kiongozi wa chama, Dkt Oburu Oginga, pamoja na kamati husika za ODM ili kutafuta suluhu kupitia mazungumzo.

Alisema hatima ya Seneta Sifuna sasa iko mikononi mwa Dkt Oginga, ambaye Kifungu cha 16(1)(g) cha Katiba ya ODM kinampa mamlaka ya kuwezesha utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala.

“Kiongozi wa chama anaombwa atumie mamlaka hayo kulinda chama na wanachama wake ambao wamekuwa wahanga wa mashambulizi yaliyokuwa kiini cha malalamishi,” ilisema sehemu ya barua hiyo.

Barua hiyo fupi na ya moja kwa moja ilikuwa tofauti kabisa na ile ya Jumatatu, ambayo ilikuwa imeeleza kwa kina sababu za kutaka Seneta Sifuna avuliwe nyadhifa zake chamani.

Katika barua ya awali, Seneta Oketch alikuwa ametaka ODM ianze mara moja mchakato wa kinidhamu dhidi ya Katibu Mkuu kwa tuhuma za utovu mkubwa wa nidhamu, kwa nia ya kumfukuza chamani.

Alimshutumu Seneta Sifuna kwa kutwaa mamlaka ya kiongozi wa chama kwa madai ya kujadiliana kuhusu miungano, kuhujumu juhudi za chama kufikia malengo yake, kukosa nidhamu na uaminifu, pamoja na kukana hadharani ushiriki wa ODM katika serikali jumuishi licha ya kuwepo kwa makubaliano ya maandishi yaliyoidhinishwa na chama.

Aidha, alimshutumu kwa kufichua taarifa za siri za chama, ikiwemo masuala ya ufadhili wa kampeni za urais za 2022, jambo ambalo alisema limeharibu taswira ya chama.

Kwa misingi hiyo, Seneta Oketch alitaka Seneta Sifuna asimamishwe mara moja, avuliwe nyadhifa zote za uongozi bungeni, au hata kufukuzwa kabisa chamani iwapo angepatikana na hatia.