Tume yaonya watumishi wa umma wanaoshiriki kampeni chaguzi ndogo
TUME ya Utumishi wa Umma (PSC) imeonya kuwa itawachukulia hatua za kinidhamu makatibu wa wizara na maafisa wa umma wanaojihusisha na kampeni kabla ya chaguzi ndogo zijazo.
Kupitia notisi iliyochapishwa Oktoba 14, 2025, Tume ilisema ni kinyume cha sheria kwa watumishi wa umma kujihusisha na siasa za vyama au kutumika kama maajenti kwa wanaogombea viti kwenye chaguzi ndogo zilizopangiwa kufanyika Novemba, 2025.
Tume vilevile imeagiza idara mbalimbali na asasi za umma kuwapa barua za kujiuzulu watumishi wa umma waliopatiwa kibali cha kuwania nyadhifa za uchaguzi.
PSC ilisema maafisa hao walihitajika kujiuzulu kazi zao katika muda wa siku saba baada ya nyadhifa kutangazwa.
“Afisa yeyote atakayepatikana na hatia ya kukiuka sheria na vipengee hivi atachukuliwa hatua za kinidhamu kuambatana na sheria zilizopo kuhusu huduma hii,” inaonya notisi aliyotia sahihi Naibu Mwenyekiti wa PSC, Mary Kumonyi.
“Kulingana na Sheria ya Uchaguzi Kipengee 43(5)(A), maafisa wa umma wanahitajika kujiuzulu kazi zao katika muda wa siku saba baada ya nyadhifa kutangazwa.”
Kipengee hiki, hata hivyo, hakiathiri rais, naibu rais, mbunge, gavana, naibu gavana na diwani.Notisi hii imejiri kukiwa na mdahalo mkali kuhusu madiwani watatu wanaogombea viti katika bunge la kitaifa.
Madiwani Newton Kariuki Ndwiga (Wadi ya Muminji) na Duncan Ireri Mbui (Wadi ya Evurore) wanamezea mate kiti cha mbunge wa Mbeere Kaskazini naye David Athman Ndakwa (West Kabras) akiwania ubunge Malava.
Kipengee 12 (c) na (d) cha Sheria ya Vyama vya Kisiasa (Cap. 7D) kinasema mtumishi wa umma hapaswi kujihusisha na shughuli ya kisiasa inayoweza kutatiza au kuonekana kuhujumu msimamo wa kisiasa wa afisi husika au kutangaza hadharani kuunga mkono au kupinga chama chochote cha kisiasa au mgombea fulani katika chaguzi.
Isitoshe, Kipengee 25 (1) cha Sheria kuhusu Maslahi Yanayokinzana Nambari 11 ya 2025, 23 ya Sheria kuhusu Uongozi na Uadilifu (Cap.185 C), na Kifungu 24 cha Sheria kuhusu Nidhamu na Maadili ya Watumishi wa Umma, inakataza maafisa wa umma kushiriki siasa, kutumika kama mawakala au kupigia debe maslahi ya chama cha kisiasa au mwanasiasa katika uchaguzi.