Tunalenga kuileta mbingu duniani tunapochanga makanisani – Tangatanga
Na LEONARD ONYANGO
Kundi la Tangatanga limetetea michango ya mamilioni ya fedha ambazo wamekuwa wakitoa makanisani huku wakisema kuwa wanalenga kuleta mbingu hapa duniani.
Kundi la Tangatanga linalompigia debe Naibu Rais William Ruto kuwania urais 2022 lilishutumu wanaopinga kutolewa kwa michango makanisani huku wakisema kuwa watakumbana na ghadhabu za Mungu.
Wamepuuzilia mbali hoja ya mwenyekiti wa ODM John Mbadi inayotaka sheria kuhusu maadili ya uongozi ifanyiwe marakenisho ili watumishi wa umma wazuiliwe kutoa zaidi ya Sh100,000 katika harambee makanisani.
Mbunge wa Suba Kusini Bw Mbadi tayari amemwandikia barua Spika wa Bunge Justin Muturi akitaka watumishi wa umma wachunguzwe wanapotoa zaidi ya Sh100,000 katika harambee.
“Wanaopinga michango makanisani watakutana na ghadhabu za Mungu na watamalizwa,” akasema Dkt Ruto alipokuwa akihutubia waumini katika kanisa la Kasuku PCEA, Ol Jororok, Kaunti ya Nyandarua.
Kulingana na Bw Mbadi, watumishi wa serikali watakatoa michango ya zaidi ya Sh100,000 watatakiwa kuandikisha taarifa kwa Tume ya Maadili na Kukabiliana na Ufisadi (EACC).
“Ukituona sisi tunajenga makanisa, si kwamba tunataka kwenda mbinguni lakini tunahitaji kuleta mbingu karibu nasi. Mswada huo wa kutaka kudhibiti michango makanisani hautafua dafu kwani utakataliwa na wabunge,” akasema Bw Murkomen.