Tunateseka: Waathiriwa wa maporomoko walia misaada ikichelewa kwa siku tatu
BAADA ya maporomoko ya ardhi kutokea Chesongoch, Kaunti ya Elgeyo Marakwet mwishoni mwa wiki iliyopita, watu waliopoteza makazi walikosa chakula, maji, na misaada ya kibinadamu kwa siku tatu.
Haya yanajiri huku wahudumu wa kibinadamu wakikabiliana na changamoto kubwa kufika maeneo yaliyokumbwa na maafa.
Mvua kubwa ilizorotesha hali ya ardhi na kuharibu barabara, hivyo magari ya msaada yanashindwa kupita kupelekea wakazi msaada katika nyumba za waliowakaribisha kwa muda.
Baadhi ya waathiriwa walipoteza watu wengi wa familia nyingi, akiwemo John Khurah, aliyepoteza jamaa 11, na Selina Krop, aliyepoteza watu 5. Wawili hao ni miongoni mwa wale ambao hawakuwa wamepata msaada hadi Jumatatu jioni.
Msaada wa chakula na vifaa vingine ulianza kufika kwenye vijiji vilivyoathirwa zaidi ambavyo ni Kasegei, Kaptul, Kwemoi, na Kipkirown Jumanne, baada ya barabara moja kuweza kufunguliwa.
Ukosefu wa miundombinu na hali tete ya ardhi vilisababisha ucheleweshaji mkubwa wa msaada, huku miamba mikubwa ikiziba njia, na kufanya jitihada za uokoaji kuwa changamoto kubwa.
Wahudumu wa kibinadamu walilazimika kutembea umbali mrefu, kuvuka mito kwa usaidizi wa wakazi wanaojua eneo vizuri. Mashirika ya serikali, ikiwemo NYS na Shirika la Msalaba Mwekundu Kenya, yalianza kwa kuopoa waliokufa kabla ya kupeleka misaada. Hali hiyo pia imesababisha wasiwasi mkubwa miongoni mwa waathiriwa, wengi wakihofia usalama wa maisha na mali yao iliyobaki.
Afisa wa Kaunti anayeshughulikia Mipango Maalumu, Lawrence Mutwol, aliwataka wakazi kushirikiana na timu za uokoaji kuharakisha mchakato wa msaada, akisisitiza kuwa hali hiyo inahitaji juhudi za pamoja na za ufanisi. Alibainisha pia kuwa kuimarisha barabara na usafirishaji wa misaada ni jambo la dharura ili kuzuia madhara zaidi.
Hadi sasa, juhudi za kuokoa na kutoa msaada zinaendelea huku jamii na serikali wakijitahidi kuhakikisha kuwa waathiriwa wanapatiwa huduma muhimu na msaada wa haraka.