Tusi mtandaoni kumgharimu mwanafunzi Sh7.5 milioni
MWANAFUNZI wa Mwaka wa Tatu wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Nairobi ameamrishwa na mahakama kufidia dereva wa Nabii David Owuor kitita cha Sh7.5 milioni baada ya kupatikana na hatia ya kumtusi kupitia ukurasa wake wa Facebook.
Hakimu mkuu wa Eldoret Dennis Mikoyan alimpata na hatia Kevin Ndung’u ya kukiuka sheria za uhalifu wa mtandao na dhuluma za mtandao ya mwaka wa 2018.
Mahakama iliamuru Benard Kagia ambaye ni mmoja wa madereva wa Nabii Owour wa kanisa la Repentance and Holiness kufidiwa pesa hizo kutokana na matusi kutoka kwa Bw Ndung’u, mtumiaji wa mitandao ya kijamii miaka mitatu iliyopita.
Sehemu ya jumbe hizo ilimtaja mlalamishi kama mwanaume ambaye hakuwa na uwezo wa kumudu matakwa ya familia yake,
Vile vile mahakama iliambiwa kuwa Ndung’u alimtaja Kagia kama asiye na maadili, madai ambayo yalimfanya mkewe kumtema.
Akitoa hukumu hakimu alibainaisha kuwa matamshi hayo yalikuwa ya kudhalilisha na kudunisha mlalamishi.
“Ni bayana kuwa mlalamishi anastahili fidia kutokana na madhara ya matusi husika hivyo basi mshtakiwa hana budi kulipa sh7, 512, 700 kama fidia,” mahakama iliamuru.
Punde baada ya uamuzi huo kulitokea sarakasi kortini pale mshtakiwa alilamika kuwa pesa hizo ni nyingi na hangeweza kuzilipa huku akitaka muda wa siku 30 kushauriana na wazazi wake kubaini uwezo wa kuzilipa.