Tutashinda virusi hivi
NA MHARIRI
Janga la virusi vya corona linatishia kutumaliza, kuharibu afya yetu, uchumi na mshikamano wa kifamilia. Janga hili linatishia kuleta balaa kubwa katika siku, wiki na miezi ijayo.
Hata hivyo, hakuna kinacholainisha mienendo yetu kuliko majanga na mateso. Mashujaa wa vita hawajulikani wakati kuna amani. Ukakamavu wao hujitokeza katika uwanja wa vita.
Vita vinavyotukumba sasa havitashindwa na walio na uwezo ama mali. Kila mwanamume, mwanamke na mtoto nchini ana jukumu kubwa. Silaha zetu sio bunduki na risasi; silaha zetu ni nidhamu ya kijamii, kujitolea na kujali kila mmoja.
Kwa sababu katika Afrika watu wengi ni maskini, serikali zetu hazijali kuinua maisha ya mwananchi na mifumo ni hafifu, ‘wataalamu’ wamekuwa wakitabiri vifo vya mamilioni humu barani. Lakini, kuna sababu ambayo imetuwezesha kuendelea kuishi katika Afrika kwa maelfu ya miaka licha ya matatizo haya.
Ili kushinda janga hili ni lazima tutafute mbinu za kuendelea kuishi kama ambavyo tumekuwa tukifanya kwa miaka na mikaka.
Virusi vya corona vimebadilisha jinsi tunavyoishi, kupenda na kuonyesha mapenzi. Salamu zetu siku hizi sio zile tumezoea. Kusalimiana kwa mikono kumekuwa jambo la kutisha, kukumbatiana kunazua hofu huku tukitembea tumevaa maski. Ni lazima tukumbatie hali hii mpya ya maisha, la sivyo tutaangamia.
Mabadiliko ya kutangamana ambayo yameletwa na Covid-19 ni jambo kidogo tu ikilinganishwa na tisho la ugonjwa huu kwa watu na serikali. Kwenye ujumbe wake mnamo Jumatatu, Rais Uhuru Kenyatta alisema: “Hakuna wakati ambao maslahi ya nchi yetu kama taifa yamewahi kutishiwa kiasi hiki.”
Katika kuandaa nchi kwa mabaya ambayo yanaweza kutokea, Rais aliangazia kuhusu maisha yalivyobadilika katika muda wa mwezi mmoja uliopita: “Tumeona mabadiliko katika familia zetu, shule, maisha, jinsi tunavyoabudu, kufanya biashara na kazi. Kila Mkenya anakabiliwa na tisho la adui hatari na ambaye haonekani wa Covid-19.”
SHUJAA
Hii ndiyo sababu lazima sote tusimame kutekeleza wajibu wetu katika kupigana na adui huyu. Ugonjwa huu unatoa fursa kwetu kubadilisha matokeo yake kwetu binafsi, familia, jamii na taifa kwa jumla.
Inasemwa kuwa kizuizi kikubwa zaidi cha kuwa shujaa ni hofu ya kuonekana mpumbavu. Lakini ushujaa wa kweli ni kuondoa tashwishwi na kujua unachopasa kufanya katika kila hatua.
Katika siku chache zilizopita tumeona kwa kiasi fulani utiifu kwa kanuni za kuzuia ueneaji wa Covid-19 zilizotolewa na Wizara ya Afya. Hizi ni pamoja na kujitenga iwapo umezuru nchi za kigeni, kafyu, kunawa mikono, kuepuka kukaribiana na kuvaa maski. Kanuni hizi zinaonyesha iwapo tuko tayari kuungana kukabili zimwi la Covid-19, ama tunataka kuendelea na maisha kama kawaida na kuliacha litumalize.
Mwito mkuu sasa ni kila mmoja alinde mwingine. Kinyume na mataifa mengine duniani yanayokumbwa na janga hili, sisi tuko na bahati kwa sababu tunaweza kujifunza kutokana na wengine ambao wametutangulia.
Kanuni na maagizo ya serikali na Shirika la Afya Duniani (WHO) yametokana na utafiti wa kitaalamu kuhusu virusi hivi vinavyosambaa, na muhimu zaidi zinavyozimwa kuenea.
MAJANGA
Kama vile tumeshinda majanga mengine mengi mbeleni, umoja wetu, ubunifu na kutovunjika moyo kumeonekana katika janga la sasa.
Mombasa watu wanapiga foleni kuchangia hazina ya dharura, Kibera kuna kijana David Avido ambaye anashona na kuwapa wakazi maski bila malipo, huku Kisumu kundi la kijamii mtaani Obunga linaongoza juhudi za usafi na uhamasishaji. Watu hawa pamoja na wengine wengi wameonyesha kuwa kila mmoja wetu ana fursa ya kuwa shujaa kwa kujitolea.
Tunapojikaza kupigana na zimwi la Covid-19, lazima tuweke macho yetu mbele ili kupata picha ya hali itakavyokuwa katika nchi yetu tuipendayo baada ya kushinda vita hivi. Kama wanajeshi wanaotoka vitani, tutakuwa tumedhoofika kwa majeraha ya kimwili na kihisia. Tayari kila mmoja ameanza kuhisi makali ya vita hivi.
Mataifa yanayostawi kama Kenya ndiyo yatagongwa zaidi na janga hili na kwa muda mrefu. Kama Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus alivyosema, mataifa yote, makampuni na mashirika ya utafiti sharti yatafute njia za kusambaza data, sayansi na ushirikiano ili watu wote wanufaike kutokana na sayansi na utafiti.
Licha ya kuwa wasimamizi wa biashara kubwa na wanasiasa watatoa mwelekeo wa sera, hali ya baadaye itategemea wananchi wa kawaida mijini na mashambani. Cha kutia moyo ni kuwa historia imeonyesha tuko na uwezo wa kushinda majanga.
Kipindi hiki pia kimeonyesha aibu ya mfumo mbaya wa afya nchini. Kwa mfano inatisha kuwa katika nchi ya takriban watu milioni 50, kuna vitanda 500 pekee vya ICU, na zaidi, miaka minane baada ya ugatuzi kuanza kuna kaunti ambazo hata hazina kitanda kimoja cha ICU.
Hii inaonyesha kuwa ni lazima tuangazie upya jinsi fedha za umma zinavyotumika na kupatia mpango wa Afya kwa Wote (UHC) msukumo mpya. Ni dhahiri kuwa viongozi wetu wamejua kuwa dunia ni kijiji kidogo ambapo maradhi yanayozuka China yanaweza kuwafanya kushindwa kwenda hospitali ng’ambo.
UCHUMI HATARINI
Huku uchumi wa dunia ukiwa hatarini, serikali za mataifa mengi zimetangaza mipango ya mabilioni ya pesa ya kuokoa sekta zilizoathirika zaidi na janga la Covid-19. Mfano ni shirika la ndege la Kenya Airways ambalo ndege zake zimekosa kazi.
Shirika la Fedha la IMF limeonya kuwa madhara ya kiuchumi yatakuwa mabaya zaidi kuliko mfumuko wa kifedha wa 2008. Kwa mfano katika muda wa wiki mbili watu milioni 10 nchini Amerika wamejiandikisha kwenye mpango wa wasio na ajira. Hili ni jambo ambalo halijawahi kushuhudiwa.
Hivyo ni dhahiri kuwa Kenya inafaa kuanza kuangazia njia za kuokoa sekta zilizoathirika zaidi. Licha ya kuwa Rais Uhuru Kenyatta ametangaza hatua kadhaa, huenda zisiwe na manufaa ya muda mrefu. Wanauchumi wametabiri kuwa watu wengi watapoteza ajira huku makampuni mengi yakipata hasara kubwa.
Huu ni wakati wetu kuwa Wakenya wazalendo kwa kuishi kwa azma za waanzilishi wa taifa hili, na kuungana dhidi ya janga hili huku tukiendelea kuwa na matumaini.
Pamoja tutashinda!