Ubabe wa Uhuru na Gachagua Mlimani tishio kwa upinzani
MUUNGANO wa Upinzani unakumbwa na jaribio lake kubwa zaidi hadi sasa, vita kati ya wafuasi wa kiongozi wa Wiper Patriotic Front Kalonzo Musyoka na wale wa Naibu Kiongozi wa Jubilee Fred Matiang’i na kuanika mgogoro kati ya vinara hao.
Kilichoonekana kama ushirikiano dhidi ya utawala wa Rais William Ruto, sasa kimegeuka kuwa mzozo mkali wa ndani kwa ndani, huku upinzani ukigawanyika kati ya kundi linalompigia debe Kalonzo linalotiwa moyo na aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua na jingine la Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, linalomuunga mkono Dkt Matiang’i.
Kauli ya hivi majuzi ya Bw Gachagua kwamba Musyoka ni ‘chaguo bora” la upinzani limechochea mvutano mpya katika muungano huo.Muungano wa Upinzani ambao unajumuisha Wiper ya Musyoka, DCP ya Gachagua, PLP ya Martha Karua, DP ya Justin Muturi, Jubilee ya Kenyatta, DAP-K ya Eugene Wamalwa na PNU chake Peter Munya, ulianzishwa kwa msingi wa malalamishi ya pamoja dhidi ya utawala wa Kenya Kwanza na haja ya kumtangaza mgombea mmoja wa urais.
Hata hivyo, kauli ya Gachagua ya kumuunga mkono Musyoka inaonekana kuuvunja na kusababisha mikutano miwili tofauti Alhamisi iliyopita kabla ya sherehe za Siku ya Jamhuri.Katika mahojiano na Taifa Jumapili, Martha Karua alisema hakuwa na habari yoyote kuhusu mpango wowote wa kumtangaza Musyoka kuwa mgombea wao wa urais, huku akisisitiza kuwa mashindano ni muhimu.
“Binafsi, sihusiki na mpango huo,” alisema kuhusu kauli ya Gachagua kuidhinisha Musyoka.
“Lakini mwanachama au wanachama wa muungano wa upinzani wana haki ya kupendekeza mtu. Msimamo wa pamoja utatangazwa kadri uchaguzi unavyokaribia. Kwa sasa mimi na wengine tunajenga majina yetu kama inavyotokea katika mashindano ya kidemokrasia.”
Katika kambi ya Musyoka, kuna hali ya kujiamini – lakini pia kuna shaka kuhusu uingiliaji unaoonekana.Mwandani wa Kalonzo, Seneta wa Kitui Enoch Wambua, mmoja wa watetezi wakuu wa Musyoka, anachukulia mvutano unaoendelea kama njama ya makusudi kutoka kwa wapinzani wao.
Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni anajitenga na “maamuzi ya siri” kuhusu mgombea wa urais.
“Katika Jubilee wito wetu mkuu ni, wacha watu waamue,” alisema.
“Kama Katibu Mkuu wa Jubilee sijawaona nyaraka zozote kuhusu mgombeaji. Bado ni mapema sana. Maamuzi haya ni bora kufanywa siku chache kabla ya uchaguzi.”
Aliongeza “Uamuzi kuhusu nani atakuwa mgombeaji wa urais lazima ufanywe na watu wengi. Hauwezi kuwa matokeo ya mkutano au vyama viwili tu. Raila alifariki akipigania demokrasia ya vyama vingi. ”
Kauli zake hazikupokelewa vizuri na viongozi kutoka Wiper na DCP, ambao wanashutumu Jubilee kwa kuwa na ndimi mbili.
“Tabia ya Jubilee ni kwamba ina mguu mmoja katika upinzani na mguu mmoja serikalini,” anasema Seneta wa Makueni Dan Maanzo. “Wanapaswa kujadili badala ya kulazimisha mambo yao. Hata walipoteza wabunge wao wote kwa Ruto.”