Habari

Ubomoaji Kariobangi Sewage wawaacha wengi bila makazi

May 4th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

CHARLES WASONGA na GEOFFREY ANENE

WAKAZI wa mtaa wa mabanda wa Kariobangi Sewage wameishutumu serikali kwa kile walitaja kutendewa unyama baada ya kuachwa bila makao kufuatia ubomozi uliofanywa majira ya alfajiri Jumatatu.

Wengi walipiga kelele nyumba zao zilipokuwa zikibomolewa na kulaani walioendesha matrekta yaliyofanya ubomozi wakisema kuwa “walijifanya kama kwamba si wazazi”.

Wakazi hao walilia wakisema hawaamini wamefurushwa kutoka eneo ambako wamekuwa wakiishi tangu mwaka 1996.

“Sisi ndio wamiliki halisi wa ardhi hii ya ukubwa wa ekari 10 yenye nambari 87. Tulipewa ardhi hii ni aliyekuwa Meya wa Nairobi Dick Waweru mnamo 1996 kama kundi la Kariobangi Farmers Sewerage Self Help Group na tukaikata kwa ploti ndogondogo miongoni mwa wanachama wote 360,” akasema Katibu Mtendaji muungano huo John Aganda Magomere.

Mwenye kofia ni Katibu Mtendaji wa Muungano wa Kariobangi Sewerage Farmers Self Help Group John Aganda Magomere akiongea na wanahabari Mei 4, 2020, baada ya wao kufurushwa na matingatinga yaliyokodiwa na kampuni ya Maji ya Nairobi (NCWSC) inayodai kuwa mmiliki wa ardhi walikojenga makao. Picha/ Charles Wasonga

“Lakini tulishangaa kwamba Kampuni ya Maji na Maji taka ya Nairobi (NCWSC) inadai ndio wamiliki hali na walitaka tuondoke. Ndipo tukawasilisha kesi kortini kupitia wakili John Khaminwa na tukapata kibali cha kuendelea kuishi huku kesi ikiendelea,” akaongeza huku akituonyesha nakala ya amri ya mahakama iliyotolewa na Jaji S. Okong’o wa Mahakama ya Milimani, Nairobi.

Lakini, anasema, Jumapili walishangaa walipopewa muda wa saa 24 kuondoka kwani kampuni hiyo “inataka kutumia ardhi hiyo”

Hata hivyo, baadhi ya wakazi Jumapili walisema waliokuwa tayari kuhama wala si chini ya saa 24 walivyoamriwa.

Mnamo Jumapili, diwani wa eneo hilo Julius Maina alisema ni aibu kubwa serikali ya Rais Uhuru Kenyatta ikiongozwa na Chama cha Jubilee inawafurusha watu kutoka makazi yao wakati huu mgumu wa janga la corona.

“Naaibika kuwa MCA kutoka Jubilee. Badala ya kusaidia watu kupata vyakula na mahitaji mengineyo wakati huu wa virusi vya corona, serikali inahangaisha wakazi. Imesahau tulikuja hapa mwaka 2013 na 2017 kuomba kura zenu na mkatupitisha,” alisema Maina akishangaliwa na wakazi hao.

Hata hivyo, baadhi ya wakazi wenye hasira walishtumu Bw Maina wakisema hakujitokeza wakati walimhitaji zaidi.

Naye Ann Mbugua kutoka shirika la kutetea haki za binadamu la Kiambu aliambia Taifa Leo katika mahojiano jana kuwa ubomozi huo uliendeshwa kinyume na sheria kwa sababu wakazi hao walikuwa wamepata agizo kutoka kwa mahakama wasiodolewe mahali hapo hadi kesi yao itakaposikizwa Mei 7.

“Naamini wakazi hao watapata haki kwa sababu wana stakabadhi halali za kuishi katika eneo hilo la Kariobangi Sewage. Watarudishiwa makao yao na korti,” akasema.

Hata hivyo, mamia ya wakazi walionekana kusalimu amri walipobeba mali yao kwa kutumia malori, magari ya aina ya pick-up, mikokoteni na pikipiki na kuhamia kwingineko. Walisababisha msongamano mkubwa wa magari kwenye barabara ya Komarock Road karibu na lango la kuingia Kariobangi Sewage linalopatikana katikati ya mtaa wa Kariobangi North, soko la Korogocho na viwanda wa Kariobangi Industries.

Kodi ya nyumba Kariobangi Sewage huwa kati ya Sh1,500 na Sh2,000. Watagharimika zaidi ya maradufu kupata nyuma katika maeneo mengine ya karibu.

Baadhi ya wakazi wameapa hawataenda kokote.

“Tutajenga nyumba, hata kama ni zitakuwa za karatasi,” alisikika mkazi mmoja akisema.

Huenda polisi walifahamu mpango kama huo kwa sababu pia walisema kuwa hawataondoka eneo hilo hadi wahakikishe kuwa ubomozi umekamilika.

Buldoza mbili zilitumiwa kubomoa makazi hayo, huku moja ikionekana ikichumba mtaro, ishara kuwa huenda eneo hilo likawekwa ua.

Trekta la nne lilikuwa kwenye kona kabisa katika mtaa huo likiondoa jaa la taka.