UCHAGUZI MIGORI: Obado ampa Raila wasiwasi
Na WAANDISHI WETU
GAVANA Okoth Obado wa Migori amemtia wasiwasi kiongozi wa ODM Raila Odinga licha ya kuwa korokoroni kwa uwezekano wa kumuiaibisha kwa mara nyingine katika siasa za kaunti hiyo na Nyanza kwa jumla.
Mara hii ubabe wa wawili hao utapimwa Jumatatu kwenye uchaguzi mdogo wa useneta katika Kaunti ya Migori, ambako chama cha ODM kimejipata kikikabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa kijana Eddy Oketch, 27, anayeungwa mkono na Bw Obado.
Bw Obado, ambaye amekuwa akipinga hatua za kisiasa za Bw Odinga katika kaunti hiyo kwa miaka mingi, amekuwa kizuizini kwa zaidi ya wiki mbili sasa na anatarajiwa kortini leo akitumaini kupewa dhamana kwenye kesi ya mauaji ya mpenzi wake, Sharon Otieno.
Ingawa yuko kizuizini, Bw Obado angali na ushawishi huku wafuasi wake, marafiki na maafisa wa kaunti wakielezwa kuunga mkono Bw Oketch.
Gavana huyo amekuwa akiwahimiza wakazi wampigie kura Bw Oketch, wa chama cha Federal Party of Kenya (FPK), licha ya kuwa yeye alichaguliwa kwa ODM. Alichukua hatua hiyo ya kukaidi chama chake akipinga hatua ya ODM kumpa tiketi ya moja kwa moja hasimu wake wa muda mrefu kisiasa, Bw Ochillo Ayacko.
“Siwezi kuunga mkono uamuzi unaofanywa na watu wachache kwenye chumba cha mikutano Nairobi,” alisema Bw Obado mnamo Julai.
Bw Odinga kwenye kampeni za Bw Ayacko alifafanua kuwa walimpa kura ya moja kwa moja kutokana na kura ya maoni iliyoonyesha alikuwa maarufu zaidi. Awali ilionekana ingekuwa mteremko kwa Bw Ayacko, ambaye pia Jubilee ilisema inaunga mkono, lakini siku za mwisho mwisho ilibainika Bw Oketch alikuwa na uungwaji mkono mkubwa.
Umaarufu wa Bw Oketch umemtia wasiwasi Bw Odinga kuhusu uwezekano wa kuaibishwa tena na Bw Obado, na ndiposa kwa siku kadhaa kabla ya uchaguzi wa leo alipiga kambi Migori akiandamana na wakuu wa ODM kuwashawishi wakazi kumchagua Bw Ayacko.
Tangu 2013, Bw Obado amedhihirisha ndiye kiboko cha Bw Odinga eneo la Nyanza kwa ukaidi wake. Mwaka huo, gavana huyo alihama ODM akilalamikia ubaguzi katika kura ya mchujo, akawania ugavana kupitia chama kidogo cha People’s Democratic Party na akashinda, katika tukio ambalo halikutarajiwa eneo hilo.
Bw Obado alidai ODM kilimpendelea Prof Edward Akong’o Oyugi kushinda tiketi kwenye mchujo. Ingawa ushindi wake ulifutiliwa mbali wakati Prof Oyugi alipolalamika kortini, gavana huyo aliibuka tena mshindi pale Mahakama ya Juu ilipoamua mahakama ya rufaa ilikosea ilipofutilia mbali ushindi wake.
Mwaka jana ODM kilisimama nyuma ya Bw Ayacko kushinda tiketi ya ODM na kikatuma vigogo wake wakingozwa na Gavana wa Mombasa Hassan Joho kumpigia debe, lakini Bw Obado alishinda mchujo na hatimaye uchaguzi wa ugavana.
Wakati ODM kilipoteua Bw Ayacko moja kwa moja kuwania useneta kufuatia kifo cha Ben Oluoch, Bw Obado alipinga mara moja hatua hiyo na akaamua kwenda kinyume cha msimamo wa Bw Odinga kwa kumuunga mkono Bw Oketch.
Wasiwasi wa ODM kuhusu uwezekano wa kiongozi wao kutiwa doa na Bw Obado, ulijitokeza kwenye kampeni wikendi hii wakati wakereketwa wake walipoeleza waziwazi kuwa kinyang’anyiro hicho ni kumhusu Bw Odinga.
Mwenyekiti wa ODM, Bw John Mbadi, alisema ni lazima chama chake kishinde uchaguzi huo kwa ajiri ya Bw Odinga. “Huu uchaguzi unamhusu Raila Odinga. Ni lazima tuthibitishe uzalendo wetu na uaminifu kwake kwa kumpigia kura Bw Ayacko. Lazima tuonyeshe dunia nzima kwamba ngome yake ingali imara,” akasema Bw Mbadi.
Mnamo Ijumaa, Bw Odinga mwenyewe aliwasihi wakazi wa Migori wasimuaibishe: “Kwa kumpigia Ayacko kura mnaniunga mkono. Tafadhali msiniaibishe.”
“Bw Ayacko lazima ashinde kiti hiki ili Bw Odinga azidi kushikilia sifa yake kama kigogo wa kisiasa katika eneo hili. Bila ushindi huu, matokeo yoyote tofauti yatamharibia sifa Bw Odinga,” akasema mchanganuzi wa siasa, Bw John Oyoo.
Hata hivyo, itakumbukwa kwamba ODM hakijawahi kushindwa kwenye uchaguzi wowote mdogo katika eneo la Nyanza.
Bw Ayacko alipuuzilia mbali dhana kwamba hatua ya Bw Odinga na viongozi wengine wakuu kukita kambi katika kaunti hiyo wiki iliyopita ilitokana na kuwa wanahofia umaarufu wa Bw Oketch katika eneo hilo.
“Hali ya kwamba viongozi wakuu wa ODM walikita kambi hapa kunifanyia kampeni haimaanishi kwamba tunamwogopa. Ninatoa wito kwa wakazi wa Migori wajitokeze kwa wingi kupiga kura,” akasema Bw Ayacko.
Mbali na kupata uungwaji mkono kutoka kwa gavana wa eneo hilo, Bw Oketch, pia alipigiwa debe na Mbunge wa Kuria Magharibi Mathias Robi aliye katika Chama cha Jubilee, na Solomon Hodo aliyekuwa akiwania kiti hicho kupitia People Democratic Party lakini akajiondoa dakika za mwisho. Bw Hodo alikuwa mgombeaji pekee kutoka jamii ya Wakuria, ambao wengi wao wamekuwa wakivuta upande wa Jubilee.
Wagombeaji wengine wanaomezea mate kiti hicho ni Bw Jobando Peter Osieko wa Green Congress Party, na wagombeaji huru Ogola Dickson na Otieno Samuel Otieno.
Kamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Prof Abdi Guliye na Kamanda wa Polisi wa eneo hilo, Bw Leonard Katana, jana walihakikishia wakazi kwamba maandalizi yote yamekamilika, na wakatakiwa kujitokeza kutekeleza haki yao ya kikatiba kwa kumchagua seneta mpya.
Bw Katana alisema kulikuwa na amani wakati wote wa kampeni na visa vidogo vilivyotokea vikadhibitiwa kwa haraka.
“Tumeorodhesha maeneo ambako kuna uwezekano wa fujo na kutakuwa na usalama zaidi katika maeneo hayo,” akasema.
Imeripotiwa na Valentine Obara, Vivere Nandiemo, Elisha Otieno, Ruth Mbula na Victor Otieno