Habari

Uchaguzi Mkuu kuandaliwa 2026? Mtaalamu wa sheria anaamini hivyo akitoa sababu hizi…

Na NIVAH KIRIMI April 25th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KATIKA tafsiri ya kipekee ya Katiba ya Kenya, mtaalamu wa sheria ya uchaguzi anapendekeza kuwa uchaguzi mkuu ujao unapasa kufanyika 2026 na sio 2027.

Wakili mashuhuri Willis Otieno anasema kwamba, uchaguzi mkuu wa urais ujao unafaa kufanyika Agosti 2026, badala ya 2027 kama inavyopangwa.

Akirejea vifungu vya katiba na maamuzi ya awali ya mahakama, Bw Otieno anadai kuwa, taifa limekuwa likitafsiri vibaya vipindi vya mihula ya rais tangu Katiba ya 2010 ianze kutumika.

“Naleta pendekezo hili nikitambua jukumu la kutetea katiba. Nawaomba Wakenya watekeleze masharti ya katiba kwa uaminifu,” alisema Bw Otieno akizungumza katika kipindi cha Fixing the Nation kwenye runinga ya NTV.

Msingi wa hoja ya wakili Otieno ni kwamba, Katiba ya 2010 iliondoa dhahiri kifungu cha awali kilichotoa muda wa miaka mitano wa muhula wa urais. Badala yake, anasema katiba ya sasa inahitaji uchaguzi kufanyika “katika mwaka wa tano, si baada ya mwaka wa tano” wa muhula wa rais.

“Tunahitaji kuamka kutoka kwa kile ninachokiita uvivu wa kitaifa na kuachana na mawazo yaliyobaki kutoka katiba ya zamani,” alisisitiza Bw Otieno.

Alitoa mfano wa muhula wa kwanza wa Rais wa zamani Uhuru Kenyatta, uliodumu kwa miaka minne na miezi mitano badala ya miaka mitano kamili, kama ushahidi kwamba, katiba haijahakikisha muhula wa miaka mitano wa rais.

Wakili huyo alirejelea hasa Kifungu cha 177(4), ambacho kinawapa Wawakilishi wa Wadi katika mabunge ya kaunti muda wa miaka mitano kamili, kipengele ambacho anasema hakihusu urais.

Alinukuu kesi katika Mahakama ya Rufaa ambapo Wawakilishi wa Wadi walipinga kukatizwa kwa mihula yao kwa sababu ya uchaguzi uliopangwa kabla ya kumalizika kwa kipindi chao cha miaka mitano. Mahakama iliamua kuwa ingawa MCAs wanastahili muhula wa miaka mitano, hitaji la kikatiba la kufanyika kwa uchaguzi Jumanne ya pili ya mwezi Agosti katika mwaka wa tano linapewa kipaumbele.

“Mahakama ya Rufaa katika uamuzi wake ilieleza kwa usahihi mwaka wa tano, ulipoanza na ulipoisha,” alieleza Bw Otieno.

Anasema kuwa ingawa maamuzi ya awali ya mahakama yalihusu uchaguzi wa 2022 pekee, suala la uchaguzi wa 2026 linawakilisha hatua mpya ambayo bado haijafikishwa mahakamani.

Wakili Otieno alipuuzilia mbali wasiwasi kuhusu athari za bajeti, akibainisha kuwa Kenya tayari hufadhili tume ya uchaguzi kila mwaka.

“Athari za bajeti si za kipekee. Hizi ni gharama za kawaida ambazo watu wa Kenya hukubali kila wanapotakiwa kukabidhi mamlaka yao ya kikatiba kwa wawakilishi waliowachagua kidemokrasia.”

Tafsiri hii ya ujasiri ya kikatiba huenda ikachochea mjadala mkubwa miongoni mwa wataalamu wa sheria, wachambuzi wa kisiasa, na umma kwa ujumla kadri Kenya inavyokaribia msimu mwingine wa uchaguzi.

Ikiwa tafsiri ya Otieno itapata uungwaji mkono, huenda ikabadilisha kwa kiasi kikubwa mwelekeo wa kisiasa wa taifa kwa kuleta uchaguzi wa urais kufanyika mwaka mmoja mapema.