Uchungu wa familia iliyopoteza jamaa wanne ajalini
FAMILIA katika eneo la Rabai, Kaunti ya Kilifi yaomboleza jamaa wao wanne waliofariki kwenye ajali iliyotokea Jumapili eneo la Kanga lililo Mtito Andei, kwenye barabara kuu ya Nairobi-Mombasa.
Kwenye mahojiano Jumatatu, Bw Mwatsuya Mutsunga alishindwa kuzuia machozi akieleza kuhusu msiba uliokumba familia yake.
“Nianze kumwomboleza nani?” aliuliza kwa sauti ya chini iliyotetemeka kwa huzuni. “Mwanangu? Kaka yangu mkubwa? Mke wake? Au mwana wao pia ni damu yangu? Mtu anaanzaje kuomboleza watu wengi namna hii? Na baada ya machozi kukauka, nitawaambia nini waliosalia kama mzee wa familia hii?” aliuliza.
Familia yake ni miongoni mwa zilizoathiriwa zaidi na mkasa huo ambao umegusa eneo la Pwani na kitaifa.
Basi lililokuwa limebeba karibu abiria 50, wakiwemo zaidi ya wachungaji na waumini 12, liligongana ana kwa ana na lori kubwa la mizigo walipokuwa wakirejea Mombasa kutoka mazishi yaliyofanyika Lugari, Kaunti ya Kakamega.
Ajali hiyo ilisababisha vifo vya watu 24. Miongoni mwa waliofariki ni kaka mkubwa wa Bw Mutsunga, Dkt Patrick Mutsunga; mkewe, Younitta Mutsunga; mtoto wao, Ndune Mutsunga; na mwanawe Mutsunga, Moses Mwadzuya.
Bw Mutsunga, alisema jioni ya Jumapili ilikuwa ya uchungu kwake huku taarifa za vifo hivyo zikimfikia moja baada ya nyingine.
“Nilipigiwa simu ya kwanza saa moja usiku hivi. Mwanzoni tuliambiwa kuwa kaka yangu mkubwa alikuwa amefariki papo hapo, huku mkewe akifariki alipokuwa akipokea matibabu katika hospitali moja Kaunti ya Makueni. Wengine wawili walikuwa bado hawajatambuliwa,” alikumbuka.
Kabla familia haijapata muda wa kukubali taarifa hizo za kwanza, naibu chifu wa eneo hilo alifika na habari nyingine za kusikitisha kwamba miili ya Ndune na Moses pia ilikuwa imetambuliwa katika eneo la ajali.
“Tulivunjika moyo kabisa. Mwezi mmoja tu uliopita, mwanangu Moses aliondoka kijijini na kwenda Mombasa kumsaidia mkewe kutafuta matibabu. Sasa hayupo tena, akiwa ameacha mjane na watoto watatu wanaosoma,” akasema.
Kaka yake mkubwa, Dkt Patrick, alikuwa nguzo muhimu ya familia. Akiwa mtaalamu wa afya aliyestaafu, aliendesha zahanati ya kibinafsi na shule ya kibinafsi katika Kaunti ya Kwale pamoja na mkewe, Younitta.
“Alinipigia simu Jumatano iliyopita kunijulisha kuhusu safari ya kumzika shemeji yake, Askofu Isaiah Giganene,” alisema Bw Mutsunga.
Alisema alimtakia safari njema. “Sikuwahi kufikiria kwamba hiyo ingekuwa mara ya mwisho kusikia sauti yake. Sasa nimeachiwa jukumu kubwa la kuwatunza wale aliowaacha,” aliongeza.
Habari za msiba zilipoenea Rabai, wanakijiji waliacha shughuli zao za kila siku na kusaidia kuweka mahema na kukaa pamoja na mzee huyo wa familia aliyekuwa akiomboleza.
Waombolezaji walizunguka kutoka hema moja hadi jingine kuwafariji ndugu wa marehemu. Bw Tsuma Kanyonge, mzee wa familia, alisema kupoteza jamaa wanne katika ajali moja ilikuwa pigo kubwa kwa familia na jamii nzima.
“Fikiria kupoteza tawi zima la familia kwa wakati mmoja. Tutaendeleaje na maisha?” aliuliza Bw Kanyonge.
Alisema walikuwa wamesikia kupitia redio za eneo hilo kwamba kulikuwa na ajali ya magari kugongana ana kwa ana kwenye barabara kuu, lakini hawakujua kuwa jamaa zao walikuwa miongoni mwa waliokuwa ndani ya basi hilo.
“Hili ni pigo kubwa, na tunamwomba Rais William Ruto kuingilia kati na kuwasaidia watoto hawa wadogo na wajane,” alisema.
Msiba huo umeibua tena malalamishi kuhusu hali ya usalama barabarani inayozidi kuzorota katika barabara ya Mombasa–Nairobi.
Haya yanajiri wiki chache tu baada ya ajali iliyotokea Salama Oktoba 4 na kusababisha vifo vya mahujaji 17 wa Kanisa Katoliki. “Wiki mbili zilizopita tulipoteza mahujaji 17, na leo tunaomboleza wengine 23. Hali hii itaendelea hadi lini?” aliuliza Bw Kanyonge.
Alizitaka mamlaka husika kuwakamata wamiliki wa magari yasiyofaa kutumika barabarani yaliyohusika katika ajali hizo, na kutambua pamoja na kuweka alama katika maeneo yote hatari kwenye barabara hiyo ili kulinda maisha ya watu.
Mbunge wa eneo hilo, Bw Kenga Mupe, aliingilia kati Jumatatu asubuhi na kushirikiana na utawala wa eneo hilo kupanga usafirishaji wa miili ya watu hao wanne kutoka Makueni hadi chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Pandya Memorial mjini Mombasa, huku maandalizi ya mazishi yakianza.