HabariHabari za Kaunti

Wazee sasa kusaidia familia kutatua mizozo ya urithi

Na TITUS OMINDE October 28th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

FAMILIA  katika eneo la North Rift zimehimizwa kuacha mizozo ya urithi inayodumu kwa miaka mingi na badala yake kutumia upatanishi kutatua tofauti zao kuhusu mali ya wazazi wao.

Mahakama imeanza kushirikiana na wazee wa jamii kusaidia familia hizo kufikia makubaliano, kupunguza mrundiko wa kesi mahakamani na kuwezesha familia kupata mali waliyorithi kwa haraka.

Zaidi ya viongozi 60 wa jamii kutoka Baraza la Wazee wa Kalenjin wameidhinishwa na Idara ya Mahakama kuendeleza Mfumo Mbadala wa Kutatua Mizozo (AJS).

Wazee hao wanaripotiwa kutatua zaidi ya mizozo 1,200 kupitia upatanishi katika mwaka uliopita, mingi ikihusu migogoro ya ardhi iliyodumu kwa muda mrefu.

Jaji Charles Yano wa Mahakama ya Mazingira na Ardhi mjini Eldoret alisema kesi za urithi ni miongoni mwa sababu zinazochangia mrundiko wa kesi katika eneo hilo.

Akizungumza Jumatatu wakati wa maadhimisho ya miaka 10 ya AJS, jaji huyo alizitaka familia kutumia upatanishi badala ya kusubiri kesi mahakamani kwa miongo kadhaa.

“Ninaomba familia kukumbatia mfumo huu na upatanishi unaofanyika kwa ushirikiano na mahakama katika masuala ya urithi, badala ya taratibu za mahakama zinazoweza kuchukua miongo kadhaa,” alisema.

Aliongeza kuwa kesi za muda mrefu hugharimu familia pesa, huzidisha migawanyiko na kuwanyima warithi fursa ya kufurahia mali yao.

Baadhi ya mizozo mikubwa ya urithi inayotajwa katika eneo hilo inahusu mali za mwanasiasa na mkulima mashuhuri Jackson Kibor na John Kiplagat Kibogy. Watoto wao wamekuwa wakizozana mahakamani kwa zaidi ya miaka 10 kuhusu mali inayokadiriwa kuzidi Sh15 bilioni.

Chama cha Wanasheria nchini (LSK), tawi la North Rift, kinaunga mkono juhudi hizo na kuendesha kampeni za kuhamasisha wazee, viongozi wa dini na wadau wengine kuhusu umuhimu wa upatanishi.

Mwenyekiti wa tawi hilo, Oscar Oduor, alisema mfumo huo unaweza kusaidia familia kutatua mizozo ya urithi kwa kufuata sheria.

Mwenyekiti wa upatanishi Uasin Gishu, wakili Daniel Tariko, alisema makubaliano yanayofikiwa kupitia upatanishi unaohusishwa na mahakama yanaweza kupitishwa na mahakama kuwa amri rasmi.

Hatua hiyo inaweza kufungua njia kwa warithi kupata mali yao kwa mujibu wa sheria.

Kwa familia zinazokumbwa na mizozo, ujumbe ni kutafuta suluhu mapema kabla ya kesi ndefu kuzidisha uhasama na kuchelewesha ugavi wa urithi.