Ufisadi ni propaganda tupu – Ruto
Na WAIKWA MAINA na CHARLES WASONGA
NAIBU Rais William Ruto amepuuzilia mbali kampeni inayoendelea dhidi ya ufisadi akisema ni propaganda zinazoendeshwa na watu aliowataja kama vibaraka waliopoteza mwelekeo.
Dkt Ruto alisema Jumamosi watu hao wanaongozwa na chuki, uongo, nia mbaya ya kuwapumbaza wananchi wasione mazuri yanayofanywa na serikali ya Jubilee.
Rais Uhuru Kenyatta amekuwa akiongoza vita dhidi ya ufisadi na ameapa kwamba hatalegeza kamba.
Akiongea katika uwanja wa Rurinja, mjini Njabini, Kaunti ya Nyandarua, ambako aliapa kuendelea kuunga mkono miradi ya maendeleo ya Kanisa, Dkt Ruto alisema wale wanaopaza sauti kuhusu ufisadi serikalini, wanafaa kujadili utendakazi wa serikali na mafanikio yake.
“Wanazunguka kote nchini wakieneza propaganda kuhusu ufisadi, nawaambieni ya kwamba ni watu waovu wenye kijicho. Wanataka ionekane kana kwamba serikali haifanyi kazi na kwamba ufisadi umekithiri. Wapuuzeni kwani ni vibaraka waliopoteza mwelekeo,” Dkt Ruto alisema.
Alisema miradi yote ya serikali inaendelea ilivyopangwa na hakuna iliyokwama kwa ukosefu wa fedha.
Matamshi yake yanajiri siku tatu baada ya waziri wa fedha Henry Rotich na maafisa wakuu wa wizara hiyo kusimamishwa kazi baada ya kushtakiwa kuhusiana na sakata ya ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kimwerer. Inadaiwa Sh21 bilioni zilipotea.
“Wajibu wangu kama Naibu Rais ni kusimamia miradi hiyo na kuhakikisha imetekelezwa ilivyopangwa bila hitilafu. Tumejitolea kutimiza ahadi zetu. Wale wanaohubiri kuhusu ufisadi sharti waelewe haya. Watu wa Nyandarua na Wakenya ni mashahidi wa utendakazi mzuri wa serikali,” akasema.
Matamshi yake pia yanajiri siku moja baada ya wandani wake kutoka ngome yake ya Rift Valley pia kukejeli vita dhidi ya ufisadi wakisema vinaendeshwa kwa njia isiyozingatia usawa.
Wakiongea katika eneobunge la Kesses, kaunti ya Uasin Gishu, wabunge Oscar Sudi (Kapseret), Nelson Koech (Belgut), Hillay Kosgei (Kipkelion Magharibi), Catharine Waruguru (Laikipia) walidai “watu fulani wanasazwa” katika vita dhidi ya uporaji mali ya umma.
“Mtindo unaotumiwa hapa ni ule wa shamba la wanyama. Kuna wanyama wengine ambao ni bora kuliko wenzao…hakuna haki kwani wahusika wengine wa ufisadi bado wako huru huku Rotich na Thugge wakifikishwa kortini,” akasema Bw Kosgei.
Jana, Dkt Ruto alisema madai kuhusu ufisadi yameshamiri ungedhani serikali haifanyi kazi akiongeza kuwa, mjadala kuhusu ufisadi unalenga kuhujumu ajenda ya maendeleo ya serikali.
“Nawahakikishia kuwa Kenya iko katika mkondo mzuri, tumetekeleza miradi ya maendeleo katika pembe zote nchini,” alieleza.
Uchoyo
Kuhusu michango yake kwa miradi ya kanisa, Dkt Ruto aliwataja wanaoipinga akiwataja kama wendawazimu, wachoyo na wachawi.
“Wanaopinga michango yangu kanisani ni wachawi ambao hawawezi kufaulu kwa chochote,” akasema.
Kwa upande wake, Gavana wa Nyandarua Francis Kimemia alilalamika kuhusu ugavi wa rasilimali za kitaifa, akisema kaunti ya Nyandarua imetengwa na iko nyuma kimaendeleo ikilinganishwa na kaunti zingine za Kati mwa Kenya.
“Maji kutoka Nyandarua hutumika Nairobi, Nakuru na kaunti nyingine jirani lakini kinaya ni kwamba sisi wenyeji hatuna maji ya matumizi nyumbani na mashambani. Nyingi za barabara zetu hazina lami. Tuna miradi mingi iliyokwama ikiwemo ujenzi wa mabwawa ya Malewa na Pesi,” akasema Bw Kimemia aliyeonekana kutofautiana na kauli za Dkt Ruto.