HabariSiasa

UFISADI: Rotich atumbukia bwawani

July 23rd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na VALENTINE OBARA

SAKATA ya mabwawa ya Arror na Kimwarer katika Kaunti ya Elgeyo Marakwet, Jumatatu ilimtumbukiza Waziri wa Fedha, Henry Rotich kwenye hatari ya kupoteza kazi na kufungwa gerezani.

Hii ni baada ya Mkuu wa Mashtaka ya Umma, Noordin Haji kuagiza Bw Rotich pamoja na Katibu wa Wizara ya Fedha, Kamau Thugge na wengine akiwemo Katibu wa Wizara ya Jumuiya ya Afrika Mashariki Susan Jemtai Koech, Meneja Mkurugenzi wa Mamlaka ya Kustawisha Kerio Valley (KVDA) David Kimosop na Afisa Mkuu wa Mamlaka ya Mazingira (NEMA) Geoffrey Wahungu.

Wizara ya Fedha ni kitovu cha mipango yote ya maendeleo ya kitaifa na kukamatwa kwa waziri na katibu ni pigo kubwa kwa imani ya wawekezaji wanaochangia uchumi wa nchi.

Punde baada ya tangazo la Bw Haj, dhamana ya hati zinazotumiwa na Kenya kukopa pesa kutoka masoko ya kimataifa ilianza kushuka nchini Uingereza.

Wizara hiyo ina majukumu ya kushawishi wawekezaji na wahisani, hasa kutoka mataifa ya kigeni kufadhili miradi mbalimbali.

Waziri wa Fedha akisaidiana na katibu wake huhitajika kusimamia na kuidhinisha uundaji wa sera za kifedha zinazoongoza taifa, na vile vile kuidhinisha mapendekezo kuhusu mikopo na utumizi wa pesa za umma.

Hata hivyo, Mhadhiri wa somo la Uchumi katika Chuo Kikuu cha Nairobi, Dkt Samuel Nyandemo aliambia Taifa Leo kwamba ingawa athari za kifedha zitashuhudiwa kwa sasa, hali ya kawaida itarudi kwa vile serikali ina watu wanaoweza kuendeleza mbele kazi ya wizara.

“Hizo athari hazitadumu kwa muda mrefu. Kuna maafisa serikalini wanaoendelea na kazi, na usisahau pia kuna waziri kwenye baraza la mawaziri ambaye hana wizara yoyote anayoshikilia,” akasema, akimrejelea Bw Raphael Tuju.

Duru zilisema Rais Uhuru Kenyatta alikuwa anapanga kutangaza kaimu waziri wa fedha mara Bw Rotich atakaposhtakiwa mahakamani.

Kufikia jana jioni washukiwa walikuwa bado wanahojiwa katika afisi za DCI maeneo mbalimbali nchini. Kulingana na Bw Haji, maafisa aliotaja wakiongozwa na Bw Rotich wanapasa kuondoka ofisini mara watakapofunguliwa mashtaka.

“Ni lazima waondoke ofisini. Hawa si magavana. Nitamwandikia barua Mkuu wa Utumishi wa Umma mara moja. Sheria inahitaji ukishtakiwa na ujibu mashtaka sharti uondoke. Hata katika mataifa ya nje huo ndio mwelekeo,” akasema Bw Haji.

Wakati sakata ya mabwawa ilipofichuliwa, Rais Kenyatta alikwepa shinikizo la kuwasimamisha kazi mawaziri waliotajwa akisisitiza kuwa ni lazima washtakiwe kwanza ndipo achukue hatua dhidi yao.

Alipohutubu bungeni Aprili mwaka huu kuhusu hali ya taifa, Rais alisisitiza lazima waliotajwa watendewe haki bali wasiadhibiwe bila ushahidi.

“Wafisadi wataadhibiwa kwa misingi ya kisheria. Hatua tutakazochukua hazitategemea jinsi watu wanavyolaumiwa kabla wasikilizwe,” akasema Rais.

Mawaziri wengine waliokuwa wamehojiwa na DCI wakati huo ni Mwangi Kiunjuri (Kilimo) na Eugene Wamalwa (Ugatuzi).

“Wale tunaowashtaki leo walikuwa na majukumu ya kulinda masilahi yetu ya umma na wakakiuka imani tuliyoweka kwao,” Bw Haji alisema.

Maafisa wengi katika idara ya ununuzi ya KVDA ni miongoni mwa wanaotarajiwa kushtakiwa kuhusiana na kashfa ambapo mabilioni ya pesa yalipotea.