UFISADI: Waandamanaji Kisumu watisha kufunga ofisi za EACC
Na BRENDA AWUOR
BAADHI ya wakazi wa Kaunti ya Kisumu wametisha kufunga ofisi za Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) wakiilaumu kwa kuchelewesha pamoja na kushindwa kusukuma na kushtaki visa kadhaa vya tuhuma za ufisadi chini ya uchunguzi katika kaunti.
Aidha, wanasema inakawia na hata kukosa kubainisha majina kamili ya washukiwa wanaochangia kuzorota kwa sekta ya afya na mazingira Kisumu.
Wakazi kutoka Manyatta, Obunga, Kajulu, Bandani, Mamboleo, Nyamasaria, Ahero, Seme pamoja na maeneo mengine ya Kisumu, wakiongozwa na mwakilishi wao Bw Bonface Akach, wameonyesha ghadhabu zao wakitaka kujua sababu zinazochangia kuzorota kwa sekta ya afya na mazingira.
Wakiandamana mbele ya ofisi za EACC, Kisumu, wamesikika wakiwaita maafisa wa EACC watoke ofisini ili wawaelezee hali ya visa na ripoti kuhusu tuhuma za ufisadi ambazo wao kama tume wamekuwa wakizifanyia uchunguzi na kubaini majina ya washukiwa kwa kueleza iwapo wamefunguliwa mashtaka kortini au la.
Wametishia kufunga ofisi za EACC iwapo maafisa hawatajibu maswali hayo.
“Tume inapaswa kuelezea hali ya kesi walizofanyia uchunguzi, wabaini majina kamili ya washukiwa kwa kuelezea iwapo walifunguliwa mashtaka au la; vinginevyo tutafunga ofisi,’’ amesema Bw Akach.
Waandamanaji wakiimba nyimbo za kiharakati, wameitisha naibu mkuu wa EACC eneo la Magharibi Bw Aura Chibole, kuyajibu maswali yao la sivyo wangechukua hatua ya kufunga ofisa zao.
Bw Chibole aliyasikia maombi yao ambapo ametoka ofisini na kuyasikia malalamishi yao, lakini akawashawishi waandae orodha ya maswala ambayo walitaka majibu.
“Ni jambo zuri nyie kututembelea ofisini mwetu ila ningependa kuona orodha ya maswala yote na hasa kesi mnazotaka niangazie ofisini mwangu,’’ amesema Bw Chibole.
Bw Akach aidha, ametofautiana naye huku akisema kwamba EACC ina kesi zote kwenye faili, hivyo basi ni jukumu la Bw Chibole kupitia na kunakili kesi hizo upya.
Wakazi hao wameipa EACC muda wa siku saba kuwapa majibu yote ya maswali yao na iwapo haitatimiza ahadi, basi Jumatano wiki ijayo watafunga ofisi zote kwa sababu itakuwa ni wazi kwamba “tume imeshindwa kufanya kazi.”
“Tumewapa muda wa siku saba ambapo msipotupa majibu, tutafunga ofisi zenu,’’ ametisha Bw Akach.
Wakazi hawa wanatarajiwa kutembelea ofisi za NEMA pamoja na ofisi ya Gavana wa kaunti ya Kisumu Alhamisi asubuhi kutafuta suluhisho la malalamisho yao.