Uhaba wa mchele wanukia maji yakipungua mashambani Mwea
UENDA Kenya ikakumbwa na uhaba mkubwa wa mchele kutokana na uhaba wa maji ya kutosha katika mashamba makubwa ya mpunga kati Mpango wa Kilimo cha Unyunyiziaji cha Mwea.
Uchunguzi wa Taifa Leo umebaini kuwa mitaro ya kusambaza maji katika mashamba hayo imeanza kukauka.
Wakulima wanalalamika kuwa mpunga wao umeanza kukauka kutokana na ukosefu wa maji ya kutosha.
“Kuna maji kidogo zaidi ambayo hayatoshi kunyunyizia mashamba yetu,” mkulima mmoja alisema.
Mwenyekiti wa muungano wa watumiaji maji katika mashamba ya Mwea Peter Chege naye alithibitisha kuwa maji yamepungua kutokana na ukame wa muda mrefu.
“Ni kweli kwamba hakuna maji ya kutosha ya unyunyiziaji mashamba ya mpunga. Hata hivyo, tumeanza kutoa maji kwa mgao kuhakikisha kuwa kila mkulima anapata bidhaa hiyo kuokoa mimea yake,” akasema Bw Chege.
Mwenyekiti huyo aliwahakikisha wakulima kwamba maji yatasambazwa kwa usawa na akawataka kutokuwa na wasiwasi.
Bw Chege alisema shida hiyo imesababishwa na ukame wa kipindi kirefu.
“Tangu ukame ulipoanza, tumekuwa tukishuhudia ukosefu wa maji hali inayozua hofu,” akaongeza.
Mashamba hayo huzalisha karibu tani 113, 000 ya mchele kila mwaka na wakulima sasa wanaonya kuwa ikiwa hakutanyesha kiwango hicho cha uzalishaji kitapungua kwa hadi asilimia 50.
Mchele unaozalishwa Mwea hautoshi hitaji la kitaifa. Hii ndio maana mchele huagizwa kutoka mataifa ya kigeni ili kuziba pengo la uhaba.
Serikali inapanga kuongeza uzalishaji wa mchele maradufu kwa kupanua kuazisha kilimo cha mpunga katika eneo la ukubwa wa ekari 10,000 katika eneo la Mwea.
Wakulima pia walisema wanakabiliwa na uhaba wa maji ya matumizi ya nyumba na wakatoa wito kwa serikali kuu kuingilia kati.
“Tumekuwa tuking’ang’ania maji yaliyoko kwenye mitaro ya mashamba ya mpunga na huenda tukapatwa na magonjwa yanayosababishwa na matumizi ya maji chafu. Serikali Kuu inafaa kuanza kuwasilisha maji safi katika eneo hili kwa kutumia malori ili kuokoa maisha yetu,” mkulima mwingine alisema.