Uhaba wa vitabu wakumba mwanzo wa Sekondari Pevu
MZOZO unaohusu utekelezaji wa shule za Sekondari Pevu unazidi kuongezeka baada ya wachapishaji kuchelewesha usambazaji wa vitabu vya Gredi 10, hali inayowaacha wanafunzi wanaotarajiwa kuripoti shuleni Jumatatu bila vitabu vya kutosha.
Mnamo Jumanne, wachapishaji walisema wataanza kuchapisha vitabu hivyo mara moja, lakini wakaonya kuwa changamoto za usafirishaji zitafanya shule kupokea asilimia 50 pekee ya vitabu vinavyohitajika kufikia Januari 16.
Uchapishaji na usambazaji kamili wa vitabu hivyo unatarajiwa kukamilika Januari 31, 2026.
Kutokana na upungufu huo, wanafunzi wa Gredi 10 watalazimika kushirikiana kusoma vitabu darasani. Baadhi yao watalazimika kupokezana vitabu wakati wa masomo au kusubiri kupata nakala chache zitakazopatikana.
Wataalamu wa elimu wanaonya kuwa uhaba huo unaweza kuvuruga masomo na kuwalazimu walimu kushindwa kukamilisha mtaala ipasavyo katika wiki za mwanzo za muhula.
“Tunaahidi kusambaza angalau asilimia 50 ya vitabu vinavyohitajika shuleni ifikapo Ijumaa, Januari 16, 2026, huku lengo likiwa kukamilisha uchapishaji na usambazaji wa asilimia 100 kufikia Januari 31, 2026,” ilisema taarifa ya pamoja ya Taasisi ya Ukuzaji Mitaala Kenya (KICD) na Chama cha Wachapishaji Kenya (KPA).
Kuchelewa huko kunafuatia mvutano kati ya wachapishaji na serikali baada ya kampuni za uchapishaji kukataa kuchapisha vitabu vya Gredi 10 kutokana na deni la Sh11.4 bilioni kwa vitabu vilivyotolewa kwa Gredi 8 na 9 tangu 2022 ambalo halijalipwa.
Mvutano huo sasa unatishia kuvuruga utekelezaji wa mtaala mpya wa shule za sekondari pevu chini ya mfumo wa elimu unaozingatia umilisi (CBE).
Katika mkutano wa pamoja Jumanne, KICD na KPA walisema kuchelewa huko kunatokana kwa kiasi kikubwa na pesa hizo ambazo hazijalipwa. Mkurugenzi Mkuu wa KICD, Profesa Charles Ong’ondo, alithibitisha kuwa Wizara ya Elimu imetoa Sh5.64 bilioni ili kulipa sehemu ya deni hilo na kuwezesha uchapishaji wa vitabu.