UHASAMA wa kisiasa kati ya Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa DCP Rigathi Gachagua kuhusu udhibiti wa siasa za Mlima Kenya huenda hautaisha hivi karibuni kuelekea uchaguzi wa 2027.

Bw Kenyatta anaongoza Jubilee ambayo inamuunga mkono Dkt Fred Matiangí huku Bw Gachagua naye akisisitiza kuwa yeye ndiye ana usemi kwenye siasa za Mlima Kenya.

“Sielewi hiki chama cha Jubilee, pengine wataanza kuona kile ambacho umoja wa upinzani unakisimamia,” akasema Bw Gachagua.

Alikuwa akirejelea uchaguzi mdogo wa Narok Township ambapo DCP na Jubilee zimesimamisha mwaniaji licha ya kuwa zote ziko chini ya mwavuli wa muungano wa upinzani.

“Angalia huu uchaguzi, vyama tanzu vya upinzani vyote vimeondoa wawaniaji wao kumuunga mkono Douglas Masikonde wa DCP. Jubilee iliendelea mbele na kumsimamisha mgombeaji,” akaongeza.

Baada ya Jubilee kumsimamisha Joshua Makata, mgombeaji huyo alitangaza kujiondoa na sasa atakuwa akimuunga mkono Robert Kanyinke Kudate wa UDA.

Wawaniaji wengine ni Opondo Okupara wa Safina na Duncan D’Baba wa Vuguvugu la Kenya Moja. Kiti hicho kilisalia wazi kufuatia kifo cha Lukas Kudate wa ODM mnamo Februari 2026.

Bw Gachagua alisema kuwa licha ya Bw Kenyatta kuwaamrisha wanasiasa wa Jubilee wasimvamie, kilicho muhimu ni maelewano kuhusu jinsi ambavyo Umoja wa Upinzani utakuwa ukiendeleza siasa zake.

“Baada ya kuacha kunivamia sasa wanamlenga Kalonzo Musyoka na hawaonyeshi ukakamavu wowote katika kumpinga adui wetu ambaye ni Rais William Ruto. Wengi wa wanasiasa wa Jubilee wanawakashifu tu viongozi wa upinzani,” akasema Bw Gachagua.

Lakini Mbunge wa Laikipia Mashariki Mwangi Kiunjuri, alionekana kumkosoa Bw Gachagua, akisema kuwa siasa zake zinavumishwa tu na kisasi dhidi ya Rais Ruto baada ya kuondolewa kama naibu rais.

“Gachagua anaamini kuwa DCP ndiyo chemichemi ya demokrasia Mlima Kenya. Anaamini kuwa wote ambao hawamuungi mkono Mlima Kenya ni maadui wake na anataka hata Bw Kenyatta aonyeshe uaminifu wa kisiasa kwake,” akasema Bw Kiunjuri.

Mbunge huyo aliongeza kuwa Bw Gachagua ana tabia ya kupuuza vyama vingine vya kisiasa Mlima Kenya ndiposa amekuwa akivirejelea kama wilbaro.
Mchanganuzi wa Masuala ya Kisiasa John Okumu, anaamini kuwa kisasi cha Bw Kenyatta na Bw Gachagua ni kuhusu uteuzi wa mwaniaji wa urais mnamo 2027.
“Kenyatta hawezi kuwania urais na Gachagua bado ana nafasi. Kwa kumuidhinisha Dkt Matiangí, Bw Kenyatta ameonyesha wazi kuwa hana imani na aliyekuwa naibu rais,” akasema Bw Okumu.

Mchanganuzi huyo aliongeza kuwa Bw Gachagua ana imani na urais wa Bw Musyoka na si Dkt Matiangí ambaye anamwona kama mwanasiasa wa kugawanya ngome yake ya Mlima Kenya.