Uhasama Winnie, Oburu wakitofautiana kuhusu ushirikiano na Ruto
MWEZI mmoja baada ya kifo cha Kinara wa ODM Raila Odinga, mpasuko umeanza kuonekana katika familia yake kuhusu usimamizi wa chama na ushirikiano na Serikali Jumuishi.
Tofauti hizo zilidhihirika jana katika maadhimisho ya miaka 20 ya ODM eneo la Pwani ambapo Mbunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Winnie Odinga, alipendekeza kuwa na kikao cha kutathmini jinsi ambavyo ODM itashirikiana na Serikali Jumuishi.
Bi Winnie, mwanawe Raila alisema wakati babake alikuwa hai alikuwa mtu wa pekee ambaye alikuwa akiwakilisha maslahi ya chama kwa Rais William Ruto.
Kwa hivyo, alimtaka Kiongozi wa ODM Dkt Oburu Odinga asiwakilishe chama pekee yake katika Serikali Jumuishi akiashiria huenda jukumu hilo litamlemea na kunahitajika kuwa na mfumo unaoleweka wa ushirikiano wakati huu Raila hayuko.
“Katika suala la Serikali Jumuishi watu wa ODM waliweka imani kwa Raila katika uhusiano huu. Huu uhusiano ni mgumu na wale ambao wanausimamia sasa, wanaweza kuongoza uhusiano huu? Hili si suali ambalo nadhani naweza kulijibu,” akasema Bi Winnie.
“Naomba turejee kwa raia kupitia Kongamano la kitaifa la chama (NDC) ili tuwaone wale ambao watu watawachagua kusimamia uhusiano huu,” akaongeza Bi Winnie.
Mnamo Ijumaa, Winnie alichemsha baadhi ya wafuasi wa ODM aliposema kuna viongozi ambao wanashiriki mazungumzo usiku kwa lengo la kuuza chama na hatakubali hilo.
Mwanawe Raila, Raila Jnr naye alisisitiza kuwa yeye ndiye mkubwa wa boma la Jaramogi huku yeye akihusika na masuala yote ya nyumbani kwa Jaramogi baada ya kutawazwa msemaji wa familia ya Raila.
Alipochukua usukani, Dkt Oginga alionekana kujibu matamshi ya Bi Winnie akisema masuala aliyoyaibua watayazungumzia kinyumbani lakini hawezi kumsaliti Raila. Dkt Oginga alisisitiza kuwa ODM itaendelea kushirikiana na Rais Ruto hadi 2027.