Uhuru aambiwa 'kujitenga' kwake na Jubilee kunahatarisha siasa za 2022
Na MWANGI MUIRURI
WANDANI wa Rais Uhuru Kenyatta sasa wanalia kuwa huenda chama cha Jubilee kikaangamia mikononi mwake kwa sababu kimekosa mwongozo kutoka Ikulu.
Wanateta kuwa Rais Kenyatta, akiwa ndiye kinara wa chama hicho anaonekana wazi kuwa hana imani nacho na ameacha utovu wa nidhamu uzidi na kuvuka mipaka kiasi kwamba kwa sasa kimegeuka kuwa Mnara wa Babeli kukiwa hakuna uwiano wa lugha na mtazamo miongoni mwa wadau.
Ameonywa kuwa hatua hiyo yake ya kujitenga na mjeledi wa kinidhamu na kuhujumu mikakati ya kujenga chama kupitia kampeni za kuimarisha chama na kujenga mrithi kwa maandalizi ya mwaka 2022 kutaishia kuzama kwa Jubilee kisiasa na kijipate kikiwa hafifu katika uwaniaji wa urais.
Mbunge wa Kandara, Bi Alice Wahome ameonya kuwa matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2017 yalikuwa ya umoja wa Timu Jubilee na Timu UhuRuto, hali ambayo inafaa kuendelezwa ili kujipa guu mbele katika miradi ya kisiasa katika chaguzi zijazo.
Alisikitika kuwa Rais kwa sasa anasema kuwa hakusaidiwa kutwaa ushindi katika chaguzi za 2013 na mara mbili mwaka 2017.
“Ni makosa kusema kwamba hatukuchangia ushindi wake ilhali anajua vizuri mazingara hasi yaliyokuwa nyanjani hasa wapigakura eneo la Mlima Kenya waliokuwa wananung’unika wakihisi wametelekezwa kiuchumi,” akasema Bi Wahome.
Mbunge wa Mathira, Rigathi Gachagua naye anasema ameshtuka sana.
“Nimeshtuka sana kusikia kuwa hatukumsaidia Rais kuwindana na upinzani hadi akaibuka mshindi,” akasema Gachagua.
Bw Gachagua anasema Rais anajua vizuri kuwa katika mchujo wa Jubilee, alikaa kando na “akatuagiza tujitafutie ushindi kwanza kisha afanye kazi na wale ambao wataibuka washindi.”
Gachagua anawaza itakuwaje leo hii isemwe Rais ndiye aliwapa ushindi wakati “ni wazi kuwa ukishachaguliwa mchujo na chama ambacho ni maarufu kimaeneo, tayari asilimia 99 ya kazi ya kampeni ishafanyika ukisubiri tu kura ya mwisho ikuthibitishe kuwa mshindi.”
“Sisi tungekuwa na ukaidi kwa Rais Kenyatta, tungekuwa tunaangusha miswada yake bungeni lakini hatujafanya hivyo kamwe na ndiyo sababu nashindwa kuelewa hasira ya rais kwetu inachochewa na nini,” anasema.
Gavana wa Kiambu, Ferdinand Waititu alisema kwa sasa kuna shida kuu Mlima Kenya.
“Kwa sasa Rais amegeuka kuwa wa kutekeleza ubaguzi wa kisiasa ambapo wale walio na upinzani kwa Naibu Rais William Ruto wanapewa nafasi kuu kuzunguka Kenya wakimshambulia, lakini wa kutetea Ruto wakitakiwa wanyamaze,” anasema Waititu.
Waititu ameonya kuwa wanasiasa hawawezi kugeuzwa kuwa wa kunyamaa kwa kuwa kila siku ni siku ya kuandaa kadi za kung’ang’ania makuu ya kisiasa.
Rais ameendelea kuonywa kuwa katika siku za hivi majuzi amegeuka kuwa dikteta wa kimaamuzi na ambaye hatii mpangilio wa demokrasia ya vyama vya kisiasa ambapo amegeuza taifa kuwa lisilo na chama chochote cha kisiasa.
Ameambiwa sera yake ya kukumbatia upinzani serikalini hata ikiwa ni ya busara katika kusaka amani ya nchi, vigezo vya demokrasia ya kudumu lazima viwe ni kuweko kwa vyama vya kisiasa vilivyo thabiti.
Mbunge wa Kapseret, Oscar Kipchumba Sudi ameonya kuwa Rais Kenyatta amegeuza Jubilee kuwa mali yake binafsi na ambapo hatambui vyombo vya kufanya maamuzi.
Hili anasema linachochea wengine kusajili vyama vyao vya kisiasa ili kujipa hakikisho kuwa Jubilee ikisambaratika, watakuwa na kimbilio.