Habari

Uhuru aanza kuvumisha BBI

October 23rd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na KAMAU WANDERI

RAIS Uhuru Kenyatta, Alhamisi alianza rasmi kampeni za kuipigia debe ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI), akiitaja kuwa tiba kwa changamoto ambazo zimekuwa zikiiandama nchi kwa muda mrefu.

Rais Kenyatta aliungana na kiongozi wa ODM, Raila Odinga, kuivumisha ripoti hiyo jijini Kisumu, akisema inalenga kuwafaidi Wakenya wote, kinyume na kauli ambazo zimekuwa zikitolewa na baadhi ya viongozi kwamba lengo lake kuu ni kuwafaidi watu wachache. Rais alirejelea baadhi ya mapendekezo yaliyo kwenye ripoti kama kubuniwa kwa Hazina ya Kuzistawisha Wadi, akisema lengo lake ni kuupa nguvu mfumo wa ugatuzi wala si kuwafaidi viongozi wachache.

“Kuna makosa yoyote tukiongeza fedha zaidi kwa serikali za kaunti? Kuna makosa yoyote tukiwapa vijana muda wa miaka saba wanapoanzisha biashara zao kabla waanze kutozwa ushuru? Kuna makosa tukiwapa vijana wanaomaliza masomo yao muda wa miaka minne wajijenge kabla ya kuanza kulipa mikopo waliyotumia kugharimia masomo yao?” akauliza Rais Kenyatta, huku akishangiliwa na maelfu ya wananchi waliokuwa wamejitokeza kumlaki.

Baadhi ya mapendekezo ya ripoti hiyo ni kuongezwa kwa mgao wa fedha zinazotengewa kaunti kutoka asilimia 15 hadi 35 ya pato la jumla la taifa. Rais Kenyatta alisema kuwa bila amani na uthabiti wa kisiasa nchini, hakuna maendeleo yoyote yanayoweza kupatikana, akitaja hilo kama sababu kuu iliyowafanya kubuni handisheki na Bw Odinga.

“Nimekuwa na amani sana moyoni kwa miaka miwili iliyopita kutokana na handisheki. Kumekuwa na utulivu mwingi nchini tangu tulipoanza safari hii na ndugu yangu (Raila),” akasema.

Vile vile, aliisifia ripoti hiyo kama njia mwafaka ya kuiwezesha Kenya kutimiza Sheria ya Usawa wa Jinsia, kwani hilo limekosa kufikiwa kupitia njia zingine. Katika hatua iiliyoonekana kumlenga Naibu Rais William Ruto, Rais Kenyatta alisema viongozi hawapaswi kuipinga bila ya kuisoma.

“Inashangaza baadhi ya viongozi walianza kuipinga ripoti hii hata kabla haijatolewa. Tunapaswa kujiepusha na tofauti zisizofaa, kwa kukita hoja zetu kwa masuala yanayowaathiri Wakenya badala ya maslahi yetu binafsi,” akaeleza.

Dkt Ruto na wabunge wa mrengo wa ‘Tangatanga’ wamekuwa wakiapa kuipinga ripoti hiyo ikiwa haitaangazia maslahi ya wananchi wa “kiwango cha chini.” Dkt Ruto alikosa kuhudhuria hafla ya uzinduzi wake katika Ikulu Ndogo ya Kisii, Jumatano, ambapo badala yake alihudhuria mazishi katika Kaunti ya Uasin Gishu.

Alhamisi, Rais Kenyatta alimmiminia sifa Bw Odinga kwa “kuonyesha ukakamavu” kuhusiana na msimamo wake kuhusu ripoti hiyo.

“Ndugu yangu (Raila) ni mwanamume kamili. Amekuwa mvumilivu kwa wakati huu wote licha ya kuelekezewa kila aina ya lawama,” akasema. Bw Odinga alisema wataenda kila sehemu nchini kuivumisha ripoti hiyo.