Habari

Uhuru apiga marufuku uuzaji pombe mikahawani

July 28th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta amepiga marufuku uuzaji wa pombe kwenye mikahawa kote nchini huku akiamuru kwamba baa zote zitasalia kufungwa ili kudhibiti kuenea kwa virusi vya Covid-19.

Akitoa hotuba kwa taifa Jumatatu, kiongozi wa taifa alielezea kughadhibishwa kwake na mienendo ya watu kujiburudisha kwa vileo na hivyo kupuuza masharti ya kujikinga dhidi ya maambukizi kwenye mikahawa inayouza pombe.

Rais Kenyatta alieleza kuwa hali kama hiyo “inahujumu vita dhidi ya janga hili ambalo kwa hakika limevuruga maisha yetu kwa kiwango kikubwa.”

“Kwa hivyo, kuanzia usiku wa manane, leo uuzaji wa pombe katika mikahawa katika maeneo yote ndani ya Jamhuri ya Kenya ni marufuku kwa muda wa siku 30 zijazo,” akasema.

Vilevile, Rais Kenyatta alitangaza kuwa mikahawa sasa itafungwa saa moja usiku badala ya saa ya saa mbili za usiku ilivyo sasa.

Kiongozi wa taifa vilevile aliamuru Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai kufutilia mbali leseni za baa zote ambazo zitapatikana zikihudumu na kwamba hazitarejeshewa leseni hizo.

“Inspekta Jenerali wa Polisi pia atahitajika kuwasilisha ripoti ya kila wiki kwa Waziri wa Masuala ya Ndani Fred Matiang’i kuhusu baa zote ambazo leseni zao zimefutiliwa mbali,” akasema Rais Kenyatta.

Aliwata maafisa wa polisi kutowasaza watu wote ambao watapatikana wakikiuka masharti yote ya kuzuia maambukizi ya corona au kukiuka saa za kafyu hata kama ni wabunge.