Uhuru ataka Sonko na Badi wafanye kazi pamoja
Na CHARLES WASONGA
RAIS Uhuru Kenyatta kwa mara nyingine amewataka Gavana wa Nairobi na Mkurugenzi Mkuu wa Halmashauri ya Huduma za Nairobi (NMS) Mohammed Badi wafanye kazi pamoja ili kuimarisha huduma kwa wakazi wa Nairobi.
Rais Kenyatta ameonya kuwa malumbano ya kila mara kati ya wawili hao yanarudisha nyuma maendeleo katika kaunti hiyo.
“Wajibu wetu kama wananchi ni kutoa huduma kwa wananchi. Tuweke siasa kando ili tutekeleze yale ambayo tumechaguliwa kufanya,” akasema Jumatano katika jumba la KICC, Nairobi ambapo ameongoza hafla ya kutoa hatimiliki za vipande vya ardhi kwa wakazi wa mitaa ya mabanda.
Rais Kenyatta hasa amemshtumu Gavana Sonko kutokana na mienendo yake ya kulaani NMS kila mara.
“Jenerali Badi sio mwanasiasa. Nilimpa kazi ya kuongoza NMS na akimaliza kazi hiyo atarejea katika jeshi na kuendelea na wajibu wake wa kulinda raia,” akasema.
Tangu kubuniwa kwa NMS mnamo Machi 2020 Sonko amekuwa akimsuta Meja Badi kwa kile anakitaja ni “kushirikiana na maafisa fulani wa Serikali Kuu kuingilia majukumu ya afisi yake”.
Gavana huyo anadai kuwa kando na majukumu manne ya kaunti ambayo yalihamishwa kwa Serikali Kuu, NMS imekuwa ikiingilia majukumu kama vile ya usimamizi wa fedha ambayo sio miongoni mwa yale yaliyohamishwa.
Majukumu ambayo Sonko alipeana kwa Serikali Kuu, kwa kutia saini mkataba wa maelewano ni; Uchukuzi, Mipango na Ujenzi, Afya na uzoaji taka na usambazaji maji.
Mnamo Mei Gavana Sonko alitisha kuwasilisha kesi katika mahakama kubatilisha mkataba huo akisema ulitiwa saini pasi na kuhusishwa kwa wakazi wa Nairobi au bunge la kaunti hiyo.
Mapema Agosti Bw Sonko alidai kuwa makazi na gari rasmi la Gavana wa Nairobi, vimetwaliwa na NMS kinyume cha sheria.