Habari

Uhuru: Tuhudumie Wakenya kwanza, siasa za 2022 baadaye

July 12th, 2019 2 min read

Na PSCU

RAIS Uhuru Kenyatta amewakumbusha viongozi nchini kujitolea katika juhudi zao za kuhudumia Wakenya badala ya kuzingatia siasa zisizokuwa na kikomo.

Kiongozi wa nchi akiwa Nakuri amesisitiza kwamba wakati wa siasa utafika lakini kwa sasa shughuli za kuboresha maisha ya Wakenya ndizo zinazopaswa kupewa zingatio.

“Kama wewe ni mwanasiasa, usifikirie tu kujitajirisha wewe binafsi lakini badala yake jiulize jinsi utakavyoboresha maisha ya Wakenya,” amesema Rais Kenyatta.

Aidha, ametoa changamoto kwa wataalamu katika nyanja mbalimbali kuweka mbele huduma kwa nchi yao badala ya kuweka mbele maslahi ya kibinafsi.

“Iwapo wewe ni daktari, usiseme utangojea mshahara na huwezi kufanya kazi bila kulipwa. Kumbuka maisha ya Mkenya mwenzako ni muhimu zaidi kuliko unacholipwa,” akasema Rais.

Amesema hayo leo Ijumaa huko Mangu katika eneo la Rongai, Kaunti ya Nakuru wakati wa ibada ya mazishi ya marehemu wakili, mwanasiasa na mfanyabiashara mashuhuri Karanja Kabage.

Rais alimtaja Karanja Kabage kuwa shujaa wa Kenya aliyejitolea kuboresha nchi hii.

Ametambua marehemu Kabage kama raia aliyefanya kazi kwa bidii wakati wa uhai wake kuinua maisha ya Wakenya sio tu kupitia sekta ya bima ambako aliacha urathi mkubwa bali pia katika sekta zingine.

“Tunaweza kusema bila wasiwasi kwamba alikuwa mtu mwadilifu. Alikuwa mtu aliyeamini kufanya bidii na kupokea mapato kutokana na jasho lake. Lakini pia alijihusisha na mambo mengine ya manufaa kwa Wakenya,” amesema Rais.

Akaongeza: “Itakumbukwa kwamba alikuwa anasema hakufai kuwa na tofauti kati ya bima ya afya kwa matajiri na maskini. Ugonjwa haubagui. Hii inamaanisha, kwake bima haikuwa tu biashara lakini pia njia moja ya kuboresha maisha ya Wakenya wenzake.”

Ipo haja kuiga

Amesema iwapo Wakenya wote wangemuiga marehemu Kabage na kujitolea kufanya kazi kuboresha maisha ya raia wenzao, nchi hii ingeafikia malengo yake ya maendeleo haraka kuliko inavyotarajiwa.

“Kama sote tutakuwa wasiojipenda katika shughuli zetu mbali mbali, tunaweza kuafikia malengo yetu ya maendeleo kwa sababu inahitaji kujitolea na kutojipenda kuafikia malengo hayo,” Rais Kenyatta amesema.

Amewataka Wakenya kuishi pamoja kwa amani na kukataa ukabila, akisema hiyo ndiyo njia ya kufuata ili kustawi.

Naibu wa Rais William Ruto alimtaja marehemu Kabage kuwa mtu mashuhuri na mzalendo aliyekuwa na ushawishi mkubwa kwake.

“Bwana Karanja Kabage alikuwa mtu mashuhuri katika nyanja ya taaluma aliyotunukiwa. Tunamzika mtu mashuhuri aliyependa nchi yake,” Naibu Rais amesema.

Aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga, kiongozi wa chama cha ANC Musalia Mudavadi, Gavana wa Nakuru Lee Kinyanjui na mwenzake wa Nyandarua Francis Kimemia pia wamezungumza wakati wa shughuli hiyo.