Ukaguzi wa Madeni: Ajabu wafanyabiashara wakidai serikali Sh268 bilioni bila stakabadhi
ZAIDI ya Sh268 bilioni ambazo wafanyabiashara walioiuzia serikali bidhaa kwa mkopo wanadai hazijathibitishwa kupitia stakabadhi hitajika, kulingana na Kamati ya Kuthibitisha Madeni yanayodaiwa serikali.
Kulingana ripoti ya awali iliyowasilishwa katika Kamati Shirikishi ya Bunge la Kitaifa, baadhi ya stakabadhi zilizotumika kuwasilishia bidhaa hizo zina dosari hivyo basi madeni hayo hayawezi kulipwa.
Hata hivyo, kamati hiyo, inayoongozwa na aliyekuwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Edward Ouko, imeidhinisha malipo ya madeni ya Sh206 bilioni kati ya madeni ya Sh664 bilioni ambayo kamati hiyo imemaliza kuchambua.
Akithibitisha kiasi cha pesa ambazo wafanyabiashara wanadai serikali kufikia sasa, Waziri wa Fedha John Mbadi alisema kuwa kamati hiyo haijakamilisha kazi yake kwani imechambua asilimia 48 pekee ya madeni yaliyowasilishwa kwake.
“Kamati hiyo imepokea madai ya malipo ya kima cha Sh664 bilioni kutoka kwa watu binafsi, mashirika na kampuni. Kamati hiyo haijakamilisha kazi yake lakini kufikia sasa imeidhinisha kuwa madeni ya kima cha Sh206 bilioni ni halali na yanapasa kulipwa,” Bw Mbadi akasema.
“Kile ambacho niliwasilisha kwa kamati hiyo ya Bunge kuhusu hali ya madeni ambayo hayajalipwa ni ripoti ya mwanzo tu, kamati hiyo haijakamilisha kibarua chake,” Bw Mbadi akaeleza.
“Kufikia sasa endapo serikali ilikuwa na pesa, Sh206 bilioni zinapasa kulipwa,” akaongeza.
Kulingana na stakabadhi zilizowasilishwa mbele ya Kamati hiyo Shirikishi inayoongozwa na Naibu Spika wa Bunge la Kitaifa Gladys Boss Shollei, sekta za kaw, miundo msingi na ICT, afya, elimu, utawala na mahusiano ya kimataifa, kilimo na ustawi wa mji na usalama wa kitaifa ndizo zenye kiwango kikubwa cha malimbikizi ya madeni ambayo hayajalipwa kufikia wakati huu.
Kamati hiyo imeidhinishwa kwamba jumla ya Sh97 bilioni katika sekta ya kawi, miundo msingi na ICT, Sh41 bilioni katika sekta ya afya, Sh28 bilioni katika sekta ya Elimu na Sh20 bilioni katika sekta ya usalama wa kitaifa zilipwe.