Habari

Ukosefu wa hela wachangia shule kufungwa mapema

Na MERCY SIMIYU July 30th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

SHULE za umma kote nchini Kenya zimefungwa wiki moja kabla ya ratiba ya kawaida ya muhula wa pili, kufuatia kuchelewa kwa mgao wa fedha kutoka kwa serikali, hali iliyovuruga kalenda ya masomo na kuzua hofu kuhusu maandalizi ya mitihani ya kitaifa.

Kwa sababu ya kufungwa ghafla, wanafunzi sasa watakuwa likizoni kwa mwezi mzima badala ya wiki tatu zilizopangwa awali.

Masomo yanatarajiwa kuanza tena kwa muhula wa tatu mnamo Agosti 25.

Kwa mujibu wa Chama cha Wakuu wa Shule za Sekondari Kenya (Kessha), shule nyingi tayari zilianza kufunga wiki iliyopita na zilizobaki zinatarajiwa kufungwa kufikia leo (Jumatano).

“Shule zimefilisika na hali ni mbaya sana. Shule nyingi tayari zimefungwa, na kufikia leo, tunatarajia shule zote zitakuwa zimefungwa kwa likizo,” alisema mwenyekiti wa Kessha, Bw Willy Kuria.

“Kwa sasa, ni shule za kitaifa na zile za mkoa ndizo bado hazijafungwa, lakini hata hizo huenda zikafungwa hivi karibuni.”

Bw Kuria alisema kuchelewesha fedha kumelemaza uwezo wa shule kugharamia mahitaji ya msingi hasa katika muhula huu muhimu kwa maandalizi ya mitihani ya kitaifa ya KCSE.

“Huu ni muhula muhimu ambapo shule zinatakiwa kuandaa wanafunzi kwa mitihani ya kitaifa, ikiwa ni pamoja na majaribio ya kisayansi na ununuzi wa vifaa muhimu. Bila pesa, haya hayawezekani. Shule zinawatuma wanafunzi nyumbani, si kwa hiari, bali kwa sababu haziwezi kuendelea na shughuli,” alieleza.

Alifichua kuwa shule zimepokea takriban Sh2,300 kwa kila mwanafunzi katika muhula wa kwanza na karibu Sh3,200 katika muhula huu, kiwango cha chini sana ikilinganishwa na gharama halisi ya kuendesha masomo na maandalizi ya mitihani.

Kufungwa mapema kwa shule sasa kunaweka shinikizo kubwa kwa muhula wa tatu, ambao huwa mfupi lakini muhimu kitaaluma, kwani ni nafasi ya mwisho ya kumaliza mtaala na kufanya maandalizi ya mitihani ya kitaifa.

“Tunatarajiwa kuwalisha wanafunzi, kulipia umeme, na maji bila pesa? Hatuna chaguo. Hii inahatarisha ubora wa elimu. Tutarudi Agosti tukijaribu kumaliza mtaala mzima katika muhula mmoja si haki,” alisema kwa huzuni.

Alikosoa serikali kwa kushindwa kutoa fedha kwa wakati, akisisitiza kuwa mgao wa elimu haupaswi kucheleweshwa hadi shule zifunguliwe, kwani gharama kama mishahara na huduma zingine huendelea hata wakati wa likizo.

“Shule zinaendelea kulipa mishahara, wakati mwingine zikiwa na deni la miezi miwili, pamoja na bili za maji na umeme. Ucheleweshaji wa fedha unaleta matatizo makubwa,” alieleza.

Aliongeza kuwa baadhi ya shule zimesitisha huduma hata kufunga ofisi zao kutokana na kushindwa kugharamia matumizi ya msingi.

Kwa sasa, shule nyingi zinategemea michango kutoka kwa wazazi kugharamia mahitaji ambayo yalipaswa kufadhiliwa na serikali.

“Katika shule nyingi, hali ni mbaya. Hata karatasi za mitihani hazipo za kutosha. Hali hii haiwezi kudumu,” alisema.

Bw Kuria pia alisema serikali imepunguza mgao wa kila mwanafunzi kutoka Sh22,244 kwa mwaka hadi takriban Sh16,900.

Hii imefanya shule nyingi kushindwa kulipia chakula, vifaa vya kufundishia, na shughuli za ziada kama michezo, muziki na michezo ya kuigiza ambazo tayari zimesitishwa katika baadhi ya shule.

Wiki iliyopita, Waziri wa Elimu Julius Ogamba aliwahakikishia wakuu wa shule kuwa fedha zitatolewa katika muhula wa tatu, akilaumu kuchelewa huko kwa “marekebisho ya kifedha” yanayoendelea serikalini.