Habari

UoN yaahirisha kufunguliwa

July 17th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

CHUO Kikuu cha Nairobi (UoN) sasa kimeahirisha mipango yake ya kufunguliwa mnamo Septemba baada ya wafanyakazi watatu kupatikana na virusi vya corona.

Kwenye taarifa aliyotoa Alhamisi Naibu Chansela Prof Stephen Kiama alisema uamuzi huo ulifikiwa katika mkutano wa baraza kuu la chuo hicho (Seneti) mnamo Jumatano.

“Lengo kuu la uamuzi huu ni kulinda afya na usalama wa wahadhiri, wanafunzi na wafanyakazi wengine chuoni,” akasema Prof Kiama.

Alisema Baraza hilo litakutana baadaye kuamua tarehe mpya ya kurejelewa kwa masomo ya kawaida, yaani masomo ya ana kwa ana.

Hata hivyo, Profesa Kiama alisema mafunzo kupitia mitandaoni yataendelea na kwmba wanafunzi walioratibiwa kufuzu mwishoni mwa mwaka huu watafanya hivyo licha ya kuwepo kwa janga la Covid-19.

“Wahadhiri na wanafunzi wataendelea kutangamana kupitia mitandao inayowezeshwa na Intaneti jinsi ambavyo imekuwa ikiendelea,” akaeleza akifichua kumekuwa na changamoto kadhaa ambazo wanajizatiti kusuluhisha.

Naibu huyo wa Chansela alisema kufuatia kisa hicho cha maambukizi ya virusi vya corona kuthibitishwa chuoni humo, wafanyakazi wengi wameshauriwa wafanye kazi za masomo na utafiti wakiwa nyumbani.

“Na wale wenye umri wa miaka 58 kwenda juu wanahimiwa kuchukuwa tahadhari kubwa ili kujiepusha na maambukizi ya virusi vya corona,” Prof Kiama akaongeza.

Majuma mawili yaliyopita Waziri wa Elimu George Magoha alitangaza kuwa vyuo vikuu, vyuo vya kadri na vile vya kozi za ufundi vitaruhusiwa kuanza kufungua kuanzia mwezi Septemba, kwa awamu.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa taasisi hizo sharti ziweke mikakati ya kuhakikisha kuwa masharti ya kuzuia maambukizi ya Covid-19 yanazingatiwa na wanafunzi na wakufunzi wote.