Habari

Uongozi wa KDF wakazia wanajeshi kupata fedha za posho moja kwa moja

Na MOSES NYAMORI July 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WANAJESHI wa Kenya Defence Forces (KDF) hawataruhusiwa tena kupata moja kwa moja marupurupu ya posho, kufuatia agizo jipya kutoka kwa uongozi wa jeshi linalozuia fedha hizo chini ya mfumo mpya wa “Lipa Unapokula”.

Agizo hilo linanuia kuzuia wanajeshi kutumia posho ya chakula kama dhamana ya mikopo.

Hii ni baada ya ripoti kuonyesha kuwa baadhi ya wanajeshi walikuwa wakikosa mlo baada ya kuondolewa kwa mpango wa ruzuku ya chakula.

Posho hiyo ilianzishwa mwaka 2000 baada ya chakula cha asubuhi na cha jioni kuondolewa kambini, na imekuwa ikiongezwa kwa kuzingatia mfumuko wa bei ili kuwalinda wanajeshi dhidi ya athari za kiuchumi.

Kwa kuwa posho ya chakula ni sehemu ya mshahara wa jumla, baadhi ya wanajeshi wamekuwa wakiitumia kama dhamana ya kupata mikopo.

Hata hivyo, ilani mpya ya ndani ambayo Taifa Leo iliona inaagiza kuwa posho hiyo sasa italipwa kupitia Ushirika wa Akiba na Mikopo wa Ulinzi (Desacco), na sehemu ya fedha hiyo kufungwa ndani ya Apu ya Mlo ya KDF.

“Posho ya chakula italipwa kupitia Desacco ili kuzuia wanajeshi kuitumia kama dhamana ya mikopo,” inasema barua hiyo.

“Nusu ya posho hiyo itafungwa kwenye Apu ya Mlo ya KDF, na salio ambayo itaachiliwa mwishoni mwa mwezi.”

Vyanzo vya habari kutoka kambini vinaeleza kuwa agizo hilo litapunguza kiwango cha pesa wanachobaki nacho wanajeshi hasa maafisa wa vyeo vya chini ambao wanategemea sana posho hiyo.

KDF ilibadili rasmi mfumo wa zamani wa kifedha wa serikali kwa chakula cha mchana hadi mfumo wa lipa unavyokula mnamo Julai 1, 2025.

Hatua hiyo imeibua taharuki, hasa miongoni mwa wanajeshi wa vyeo vya chini.

Wizara ya Ulinzi inasema kuwa mabadiliko hayo yanalenga kuboresha matumizi ya bajeti na kuruhusu wanajeshi kuchagua mlo wanaopendelea binafsi.

Wanasema mpango huo utarahisisha shughuli na kuondoa hasara.

Ilani ya ndani ya Juni 23 2025, iliyosainiwa na Brigedia na Mkuu wa Usafirishaji Eric Nzioki, inathibitisha kuanza kwa utekelezaji wa mpango huo.

“Maombi yenu yafikishwe makao makuu haya kabla ya tarehe Juni 25, 2025. Kumbuka kuwa fedha zitakazopatikana kutoka kwa mtaji huu wa mwanzo zitatumika kama hazina ya mzunguko inayojitegemea, itakayosimamiwa na kamati za Lipa Unavyokula zilizoundwa kusimamia huduma za chakula kambini,” inasisitiza barua hiyo.

Hii si mara ya kwanza kujaribu kuanzisha mfumo huu. Juhudi za awali zilifeli kutokana na upinzani kutoka kwa wanajeshi.

Hata hivyo, uongozi wa KDF unasisitiza kuwa mpango wa ruzuku ya chakula ulikuwa umejaa mianya na uzembe uliogharimu serikali mamilioni.

Ili kuhakikisha utekelezaji, makamanda wametakiwa kuweka kipaumbele kuboresha kumbi za maakuli katika nusu ya pili ya mwaka wa kifedha 2024/25, uboreshaji zaidi umepangwa mwaka wa kifedha wa 2025/26.