Upinzani wakejeli handisheki kati ya Ruto na Gideon
VIONGOZI wa upinzani wakiongozwa na kiongozi wa chama cha Democratic Citizens Party (DCP), Rigathi Gachagua, jana waliingia kwa kishindo katika Kaunti ya Embu na kupuuza ushirikiano mpya kati ya Rais William Ruto na kiongozi wa Kanu, Gideon Moi, wakisema kuwa ni wa muda tu na hautabadilisha chochote kwa maisha ya Wakenya.
Walitaja muungano huo kama juhudi za ‘mtu anayehisi kushindwa’ na kuapa kumng’oa Rais Ruto mamlakani katika uchaguzi wa 2027.
Akihutubia wakazi katika mji wa Kiritiri alipokuwa akimpigia debe mgombea wa kiti cha ubunge cha Mbeere Kaskazini kwa tiketi ya Democratic Party (DP), Bw Newton Karis, Bw Gachagua alisema kuwa Rais Ruto ameishiwa na mbinu za kisiasa na sasa analazimika kutafuta usaidizi kutoka kwa watu ambao zamani walikuwa mahasimu wake.
‘Muungano huu wa Ruto na Moi ni wa kujifurahisha tu. Hauna mwelekeo wala athari yoyote. Wakenya wamezinduka na hawawezi kudanganywa tena,’ alisema Gachagua.
Viongozi wengine waliomsindikiza ni pamoja na kiongozi wa chama cha DAP-K, Eugene Wamalwa; kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka; kiongozi wa chama cha PLP, Martha Karua; Spika wa zamani wa Bunge la Taifa, Justin Muturi, Seneta wa Kirinyaga Kamau Murango na Mbunge wa Manyatta Gitonga Mukunji.
Bw Wamalwa alisema kuwa upinzani uko tayari kuungana na kuwasilisha mgombea mmoja mwenye nguvu na maono ya kweli kwa Wakenya, akisisitiza kuwa majaribio ya Rais Ruto kugawanya Mlima Kenya yamegonga mwamba.
‘Tumejifunza kutokana na makosa ya nyuma. Safari hii, hatutagawanyika. Tutakuwa kitu kimoja, na tutamshinda Ruto kwa kura nyingi,’ alieleza Wamalwa.
Bi Karua alisema kuwa umoja wa vyama vya upinzani ni wa dhati, na kwamba lengo lao kuu ni kuwaokoa Wakenya kutoka kwa hali ngumu ya maisha inayoletwa na sera duni za serikali ya sasa.
“Tumeshuhudia hali ngumu ya kiuchumi, ukandamizaji wa vijana, kushamiri kwa ufisadi na huduma duni za afya na elimu. Hatuna sababu ya kuendelea kuvumilia haya,” alisema Karua.
Kalonzo alitoa wito kwa vijana wa Gen Z kujiandikisha kuwa wapigakura kwa wingi, akisema kuwa wao ndiyo silaha ya mabadiliko katika uchaguzi wa 2027.
‘Ukombozi wa taifa hili uko mikononi mwa vijana. Msikae tu mitandaoni, jitokezeni kujisajili,’ alihimiza.
Bw Muturi alikashifu uongozi wa Rais Ruto, akisema kuwa hali ya elimu na afya imeporomoka na kuwa serikali imeshindwa kabisa kutimiza ahadi zake kwa wananchi.
Gachagua aliongeza kusema kwamba wanajipanga kwa uchaguzi wa 2027 kwa kuzingatia maslahi ya mwananchi wa kawaida, wala si kugawana vyeo au mamlaka.