Usafiri wa feri wasitishwa kwa muda maji yatulie kupisha wapiga mbizi kuopoa miili Likoni
Na SAMMY WAWERU
SHUGHULI za utafutaji wa miili ya mama na mwanawe waliozama majini Jumapili katika kivukio cha feri Likoni, Mombasa, zinaendelea.
Wakati huohuo shirika la huduma za feri, KFS, limetangaza kusitisha uchukuzi na usafiri katika kivukio hicho kwa muda wa dakika kadha ili maji yawe maenge kutoa mazingira mwafaka kwa shughuli ya uokoaji.
Video iliyosambazwa mitandaoni ilionesha gari walimokuwa Miriam Kigenda na mtoto wake wa kike Amanda Mutheu anayesemekana kuwa na umri wa miaka 4 ikizama majini.
Inadaiwa gari hilo lilirejea nyuma na kutumbukia wakati feri inavusha watu baharini kutoka ng’ambo moja hadi nyingine, mwendo wa saa kumi na mbili za jioni.
Inadaiwa licha ya walioshuhudia kupiga kamsa wakati wa mkasa huo hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa na KFS.
Mkurugenzi wa shirika hilo Bakari Gowa Jumatatu alifanya mkutano wa faragha na wadau husika. KFS baadaye ilitoa taarifa kwa vyombo vya habari ikieleza shughuli za kutafuta miili na gari hilo zimeanza, kupitia vikosi maalum, shirika la msalaba mwekundu likijumuishwa.
Bw Gowa alisema wapiga mbizi kutoka kikosi cha wanajeshi wa majini, Kenya Navy, walifanya utafutaji lakini hawakuweza kutambua lilipo gari hilo. Alikiri shirika hilo halina wapiga mbizi wake.
Hata hivyo taarifa ya KFS ilionekana kutofautiana na ya familia ya Bi Kigenda ambapo kufikia Jumatatu adhuhuri hawakuwa wamefahamishwa chochote. Walilalamika kwamba KFS na serikali ilisalia kimya juhudi za kutafuta miili ya wapendwa wao zikikosa kuonekana.
“Hatujaona hatua yoyote kuanza kututafutia wapendwa wetu tangu Jumapili. Tunaambiwa wapiga mbizi wa Kenya Navy sharti wapate idhini kutoka juu (akimaanisha wakubwa wao),” akasema mmoja wa wanafamilia.
Akizungumza na waandishi wa habari Jumanne, Bw Gowa amedokeza kwamba gari la mama huyo limeonekana likiwa kimo cha futi 75.
Awali, mkurugenzi huyo alikuwa ametangaza kuwa KFS itakodi wapiga mbizi wa kibinafsi, lakini amesema shughuli za kuokoa miili ya mama na mwanawe zinaendeshwa na Kenya Navy, wakisaidiana na wapiga mbizi wa halmashauri ya bandarini, KPA.
Kufikia sasa Wizara ya Uchukuzi haijatoa taarifa yake kuhusu mkasa huo.
Kufuatia tukio hilo, Wakenya wameendelea kueleza ghadhabu zao, wakinyooshea serikali kidole cha lawama kwa utepetevu.
“Ni huzuni na aibu kwa serikali kufikia sasa mwili wa Miriam na mwanawe Amanda haijatolewa. Tukio hilo la Jumapili linaonesha utepetevu unaozingira idara za serikali. KFS ilipata muda wa kunakili video lakini haikupata wa kuwaokoa,” Boniface Mwangi Kamau amechapisha mtandaoni.
Dharura
Boniface anashangazwa kuendelea kuwepo ofisini kwa mkurugenzi mkuu wa KFS, Bakari Gowa akimwana kama mtu ambaye hakudadarukia kuchukua hatua muhimu za dharura.
Joseph Makenge ametilia shaka utendakazi wa Kenya Navy, akidai janga la Likoni linaonesha wamezembea kazini.
“Wanaendelea kuandaa hafla ya maadhimisho ya Mashujaa Dei mama na mwanawe wakifa majini, aibu hiyo,” awacharura.
Kwa hakika ni jambo la kuhuzunisha kuona wanajeshi kutoka kitengo cha majini hawakujitokeza kwa wakati ufaao na kulingana ma Brian Mutie, mchanganuzi wa masuala ya kiusalama, iwapo maafisa hao wangechukua hatua mara moja, huenda mama na mwanawe wangeokolewa. “Ni aibu kwetu kama taifa kikosi cha aina hiyo kinachojukumika kwa majanga kama hayo kukosa kuitika tukio la dharura,” aeleza Bw Mutie.
Anasema kikosi hicho kinapaswa kuwa na boti yenye mwendo wa kasi, ikizingatiwa kuwa majukumu yao ni kuangazia masuala ya bahari hasa usalama.
“Katika karne hii ya 21 shirika la KFS linapafaa kuwa limeimarika; Liwe na meneja wa usalama na kikundi chake maalum na vifaa ili kuangazia majanga kama hayo,” apendekeza mchanganuzi huyo.
Mwaka 2017, kisa sawa na cha Jumapili kilishuhudiwa eneo hilo na hata kusababisha maafa.
Ili kuimarisha utendakazi wa shughuli za bahari, 2018 Rais Uhuru Kenyatta alizindua kikosi maalum cha usalama majini na kulinda maliasili yake, eneo la Pwani maarufu kama Coast Guard.