Habari

Usalama waimarishwa mitihani ya Gredi 6 na 9 ikianza Jumatatu

Na WAANDISHI WETU  October 24th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

USALAMA umeimarishwa kote nchini huku shule zikikamilisha maandalizi ya mitihani ya Gredi 6 na 9 itakayoanza Jumatatu.
Watahiniwa wa Gredi 6 watafanya Tathmini ya Elimu ya Msingi (KPSEA), huku wale wa Gredi 9 wakifanya Tathmini ya Elimu ya Shule za Sekondari za Awali (KJSEA).

Shule zilifanya mazoezi ya mwisho Ijumaa, ambapo wanafunzi walielekezwa kuhusu taratibu za mitihani na jinsi ya kujaza karatasi za majibu. Wasimamizi nao walipewa maelekezo kuhusu majukumu yao.

Katika Kaunti ya Uasin Gishu, Kamishna wa Kaunti Eddyson Nyale aliwahakikishia wanafunzi, wazazi na wasimamizi wa shule kuwa usalama umeimarishwa.

Alionya watu wasiohusika dhidi ya kwenda katika vituo vya mitihani.

“Timu ya usalama ya kaunti imeweka mikakati madhubuti kuhakikisha mazingira ni salama na ya amani katika kipindi chote cha tathmini,” alisema Dkt Nyale.

Mkurugenzi wa Elimu wa kaunti hiyo, David Koech, alisema mazoezi yalifanyika kwa mafanikio na watahiniwa wote waliosajiliwa walishiriki.
Alisema wanatarajia wanafunzi wote kufika kufanya mitihani Jumatatu.

Katika Trans Nzoia, Mkurugenzi wa Elimu Pamela Akello alisema mipango ya usalama imekamilika.

Huko Turkana, maafisa wa elimu wanashirikiana na maafisa wa usalama kuhakikisha wanafunzi katika maeneo yanayokumbwa na ujangili wa kutumia silaha wanafanya mitihani bila hofu.

Mkurugenzi wa Elimu Henry Lubanga alisema watahiniwa walio katika maeneo yasiyo salama watasafirishwa hadi vituo salama inapohitajika.

“Usalama wa watahiniwa katika maeneo yasiyo salama utahakikishwa. Katika baadhi ya hali, tutawasafirisha hadi vituo salama vya mitihani,” alisema.

Aliongeza kuwa magari na maafisa wako tayari, huku wazazi wakihimizwa kuhakikisha watoto wao wanafika kufanya tathmini.

Katika Shule ya Korinyang Mixed Boarding and Junior Secondary iliyoko Aroo, wasimamizi wanashirikiana na viongozi wa eneo hilo kuwatafuta wanafunzi waliokosa masomo kutokana na shughuli za uchimbaji dhahabu Kalomwae na maeneo ya mpakani.

Mwalimu mkuu Mahammud Abdullahi alisema uchimbaji huo umeathiri idadi ya wanafunzi katika madarasa yote, huku madarasa ya juu yakikumbwa zaidi na tatizo hilo.

Katika kaunti ya Baringo, Mkurugenzi wa Elimu Kipruto Kosgei alisema watahiniwa zaidi ya 17,226 wanatarajiwa kufanya KJSEA katika vituo zaidi ya 523. Magari yameandaliwa kusambaza karatasi za mitihani kwa wakati.

Kamishna wa Kaunti ya Nakuru Loyford Kibaara alisema wasimamizi wa vituo 480 wameelekezwa kulinda uadilifu wa mitihani na kuzuia udanganyifu.

Alisema kila kituo kitakuwa na angalau maafisa wawili wa polisi wenye silaha.

“Usimamizi mzuri wa mitihani ya kitaifa unategemea uadilifu wa maafisa wa usalama, wasimamizi na wasimamizi wa mitihani kwa sababu wanawasiliana moja kwa moja na watahiniwa,” alisema.

Katika kaunti ya Murang’a, kamati ya usalama na ujasusi imewaagiza maafisa wa eneo hilo kuorodhesha watahiniwa waliopotea na kuripoti dharura zinazoweza kuvuruga mitihani.

Kamishna wa Kaunti Hassan Bule alisema taarifa hizo zitasaidia kushughulikia hali kama vile kuhamisha vituo, wanafunzi wanaofanyia mitihani hospitalini au katika vituo vya kizuizini vya haki, na vitisho vya usalama.

Murang’a ina watahiniwa 25,334 wa KJSEA katika vituo 567 na 24,093 wa KPSEA katika vituo 618.

Meru imesajili watahiniwa 37,301 wa KPSEA katika vituo 954, huku 35,670 wakitarajiwa kufanya KJSEA katika vituo 827.

Katika eneo la Pwani, Kilifi inaongoza kwa idadi ya watahiniwa wa KJSEA, ikiwa na wanafunzi 49,602 katika vituo 680 vya umma na kibinafsi. Kwale ina watahiniwa 26,425, Mombasa 22,608, Taita Taveta 9,022, Tana River 5,937 na Lamu 4,064.

Wakati huo huo, Chama cha Shule za Kibinafsi nchini kimepongeza Wizara ya Elimu kwa kuweka mazingira yanayowawezesha watahiniwa na maafisa wa mitihani kujiandaa.

Willy Mbote, mkurugenzi wa Achievers Academy katika eneo bunge dogo la Kapseret, alisema shule za kibinafsi zimefurahishwa na maandalizi yaliyofanywa.