Ushindani mkali Malava Ndakwa, Panyako wakiwa sako kwa bako
UCHAGUZI mdogo wa Malava sasa unaonekana kuwa ushindani kati ya farasi wawili huku wanasiasa wakuu kutoka upinzani na serikali wakikita kambi eneo hilo kuwavumisha wawaniaji wao.
Mwaniaji wa DAP Kenya Seth Panyako na David Ndakwa wa UDA, wanapelekana sako kwa bako kwenye kura ambayo inatumiwa na mirengo yote miwili kupima umaarufu wao kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.
Kiti cha eneobunge la Malava kilisalia wazi kutokana na mauti ya Malulu Injendi ambaye alikuwa amehudumu kama mbunge tangu 2013.
Wawaniaji wengine ni Job Manyasi wa DNA, Wilberforce Tuva wa Kenya Moja kisha James Angatia na George Oyugi wa ARC na PDU mtawalia. Wengine ni Bruce Shivakale wa EPP na Benjamin Nalwa wa NUPEA.
Ushindi wa upinzani kwenye kura hiyo utafasiriwa kuwa mambo si mazuri kwa Rais William Ruto eneo la Magharibi kuelekea 2027. Upinzani ulipigwa jeki baada ya mgombeaji wa DCP Edgar Busiega kujiondoa na kumuunga mkono Bw Panyako.
Kwa upande mwingine iwapo Bw Ndakwa atashinda, basi upinzani utajikuna kichwa iwapo muungano wao unaweza kutikisa utawala wa Rais 2027.
Tayari Seneta wa Kakamega Bonni Khalwale, ameasi serikali na kuwa mstari wa mbele kumvumisha Bw Panyako, akisema kuwa wakati umefika wa eneo la Magharibi kuheshimiwa na wageni kukoma kuingilia siasa zake za ndani.
“Naamini kuwa Panyako ndiye kiongozi ambaye atazingatia na kusimamia maslahi ya wakazi wa Malava. Pia ushindi wake utafanya eneo la Magharibi liheshimiwe ili watu kutoka nje wasifikirie wanaamua mkondo wa siasa za eneo hili jinsi wanavyotaka,” akasema Bw Khalwale.
Kinaya ni kwamba Kiongozi wa DAP-K Eugene Wamalwa na Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya, nao wakionyesha uhasama wa wazi kati yao na kuendesha kampeni tofauti kwa Bw Panyako.
Hali hiyo imeibua madai ndani ya muungano wa upinzani kuwa Bw Natembeya huenda anadhaminiwa na mrengo wa serikali kusambaratisha umoja wa upinzani kwenye kura hiyo.
Naibu Gavana wa Kakamega Ayub Savula, ambaye alichaguliwa kupitia DAP-Kenya, naye anamuunga mkono Bw Ndakwa.
Wazee wa Kabras nao wameonekana wakimshabikia Bw Ndakwa baada ya kushawishiwa na msaidizi wa Rais Farouk Kibet.
Viongozi wa serikali wakiongozwa na Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi nao wanasisitiza uchaguzi wa Bw Ndakwa utasaidia eneobunge hilo kuendelea kunufaika kimaendeleo kupitia ushirikiano na serikali.
“Kufanya kazi na serikali ya kitaifa kuna manufaa yake na hakuna anayejiunga na upinzani kwa kutaka. Tayari tuko ndani ya serikali kwa hivyo tuendelee kuwaunga mkono viongozi wanaoegemea utawala wa sasa,” akasema Bw Mudavadi.
Kampeni zikichacha raia nao wamekuwa wakinufaika huku pesa zikimwagwa Malava kupitia mikutano ya kuinua makundi ya akina mama, vijana, ya kidini na makundi ya kijamii.