Ushindi wa Wamuthende wapingwa kortini siku mbili baada ya kuapishwa
WAPIGA kura wawili wa Mbeere Kaskazini wamewasilisha kesi katika Mahakama Kuu ya Embu kupinga ushindi wa Leo wa Muthende Njeru (UDA).
Wapiga kura hao, Julieta Karigi na Patrick Gitonga, wanataka kesi yao iidhinishwe kuwa ya dharura. Wanataka mahakama kubatilisha matokeo ya uchaguzi huo na kuamuru uchaguzi mpya ufanyike. Wanawakilishwa na wakili Kiragu Wathuta.
Wanadai kuwa mgombeaji wa UDA hakuwa mpiga kura aliyesajiliwa na kwamba kulikuwa na utata katika majina yake, hivyo uchaguzi haukuwa huru, wa haki wala kuaminika.
Wapiga kura hao wanasema kwamba mnamo Septemba 3, 2024, mgombeaji huyo alitia saini hati ya kubadilisha jina lake kutoka Leonard Muriuki Njeru na kuanza kutumia jina jipya la Leo wa Muthende Njeru.
Wanasisitiza kuwa Katiba inaeleza kuwa mtu anastahili kuchaguliwa kuwa mbunge tu iwapo amesajiliwa kama mpiga kura.
“Mtuhumiwa wa kwanza alitangazwa mshindi wa uchaguzi wa Mbeere North kwa jina Leo wa Muthende Njeru, jina ambalo halipo katika sajili ya wapiga kura. Jina pekee lililosajiliwa ni Leonard Muriuki Njeru ambalo tayari alikuwa amekana,” walisema katika kiapo chao.
Kwa msingi huo, wanahoji kuwa mgombeaji huyo wa UDA hakuwa mpiga kura aliyesajiliwa kwa jina alilotumia kugombea na hivyo hakustahili kuchaguliwa kuwa mbunge.
“Matangazo ya ushindi kwake kwa jina lisilosajiliwa katika sajili ya wapiga kura yanafanya matokeo hayo kuwa batili, yasiyo halali na yasiyofaa, jambo ambalo linahitaji hatua ya haraka ya mahakama,” walisema.
Mabadiliko hayo ya jina yalifanyika kabla ya kipindi cha uteuzi wa wagombeaji wa uchaguzi mdogo wa Mbeere North.
Katika kiapo chao, waliongeza kuwa licha ya jina mpya kuchapishwa kisheria, mgombeaji huyo aliwasilisha makaratasi ya uteuzi kwa kutumia jina lake la zamani, Leonard Muriuki Njeru, ambalo tayari alikuwa amekana.
Walilaumu Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) pamoja na afisa msimamizi wa uchaguzi wa Mbeere North, Bw John Mwii Kinyua, kwa kukubali na kushughulikia uteuzi wake kwa jina lisilo sahihi.
Wakimshtumu IEBC, walisema tume ilimruhusu mgombeaji mwenye majina mawili yanayokinzana kushiriki na hata kutangazwa mshindi.
Wapiga kura hao waliongeza kuwa matumizi ya majina mawili yanayokinzana kunaleta utata na kufanya uchaguzi uziweze kuthibitishwa.
“IEBC ina wajibu wa kikatiba kuhakikisha usahihi, uwazi na uthibitishaji wa uchaguzi,” walisema.
Zaidi, walisema kuwa matokeo hayawezi kuthibitishwa kwa sababu ya utata huo na kwamba uchaguzi uliathirika moja kwa moja kwa kuwa majina ya mgombeaji yaliathiri hatua za uteuzi, upigaji kura na tangazo la matokeo.
Wameomba mahakama itangaze ushindi wa mgombeaji huyo kuwa batili kwa kuwa uchaguzi haukufanywa kulingana na Katiba na Sheria ya Uchaguzi.
Bw Njeru, ambaye tayari ameapishwa kama Mbunge wa Mbeere North, IEBC na Bw Kinyua wametajwa kama washtakiwa wa kwanza, wa pili na wa tatu mtawalia.
Bw Wamuthende alishinda kwa kura 15,802 dhidi ya mpinzani wake wa karibu, Newton Kariuki (Karish) wa Democratic Party, aliyepata kura 15,308.
Bw Duncan Mbui wa Chama cha Kazi alimaliza wa tatu kwa kura 2,480 katika uchaguzi ambao UDA ilishinda kwa tofauti ndogo ya kura 494, kama alivyotangaza Bw Kinyua.