Ushirikiano kati ya TVET, viwanda waongeza ajira kwa asilimia 80
NDANI ya miezi sita pekee ushirikiano kati ya sekta ya viwanda na Vyuo vya Kiufundi (TVET) Afrika Mashariki umeongeza ajira hadi asilimia 80.
Ushirikiano huo hasa umewanufaisha wanawake, huku idadi ya wanawake ambao wamepata ajira ikipanda kutoka asilimia 51 hadi asilimia 74.
Vituo hivyo vya kiufundi 16 vinapatikana Ethiopia, Kenya na Tanzania na ni sehemu ya mradi unaofadhiliwa na benki kuu maarufu kama EASTRIP.
Kwa mujibu wa Dkt Kosam Joseph ambaye ni mshirikishi wa kieneo wa EASTRIP katika Baraza la Vyuo Vikuu Afrika Mashariki (IUCEA), vituo hivyo 16 vya TVET vinashirikiana na kampuni 500 kuendeleza mafunzo kwenye kozi zaidi ya 500 hasa katika sekta za kawi, sayansi ya kawi ya kuzalisha kupitia mvuke, uchukuzi, uchukuzi wa angani, utengenezaji wa bidhaa na hoteli.
“Ushirikiano huu ulianzishwa kuhakikisha wanafunzi wanasomea kozi ambapo wakifuzu ni rahisi kupata ajira. Kozi ambazo wanafanya zitakuwa zikikidhi mahitaji katika sekta ya ajira,” akasema Dkt Cosam.

Mkuu kituo cha mafunzo cha kuzalisha kawi ya mvuke KenGen Risper Kandie naye alisema wameanzisha kituo cha kufundisha teknolojia ya kawi.
Kule Tanzania, Taasisi ya Kitaifa ya Uchukuzi wa angani imeanzisha kozi zinazofunzwa kuhusu uchukuzi na uchukuzi wa angani ambao waliofuzu wamepewa ajira katika mashirika mbalimbali ya ndege za kieneo.
Kule Ethiopia, Taasisi ya General Windgate imepanua miopango yake ya mafunzo hasa katika sekta ya utengenezaji bidhaa ambapo waliofuzu sasa wameajiriwa katika viwanda mbalimbali.
Idadi ya wanafunzi ambao wako katika vituo hivyo 16 vya Tvet imeongezeka kutoka 6,971 hadi 57,857 ambapo 19,000 ni wanawake.