Habari

Utapigwa faini ya mamilioni kwa kumtusi mtu WhatsApp

Na JOSEPH WANGUI April 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KUMEKUWA na ongezeko la kesi mahakamani zinazoibuka kutoka kwa mijadala ya makundi ya WhatsApp, ambapo baadhi ya watu hutumia mfumo wa haki ya jinai kama chombo cha kulipiza kisasi au kutatua mizozo ya kijamii.

Mapema mwezi huu, Jaji wa Mahakama Kuu Diana Kavedza alikosoa polisi na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kwa kutumiwa kama “vifaa vya kisiasa” katika mzozo wa kibinafsi kati ya wakazi wawili wa Phenom Park Estate, Samburu Court, Lang’ata, Nairobi.

Kesi hiyo ilihusu mashtaka dhidi ya Bi Farzhan Aperera, mwenyekiti wa chama cha wakazi wa Phenom Park, aliyeshtakiwa kwa kosa la kusababisha usumbufu kutokana na mjadala ulioibuka kwenye kundi la WhatsApp la wakazi wakati ambao pia alikuwa anakabiliwa na kesi ya kijamii kuhusiana na suala sawa na hilo.

Kundi hilo lilianzishwa kujadili masuala ya mtaa na kuimarisha mshikamano miongoni mwa wakazi.Mjadala huo ulioibua kesi ya jinai ulifanyika mwezi Agosti 2023 na ulihusu masuala ya usalama mtaani.

Bi Aperera, akiwa mwenyekiti, alikuwa akiwapa wakazi taarifa kupitia kundi la WhatsApp. Mmoja wa wakazi alikasirika na kudai kuwa Bi Aperera alimdhalilisha kwa jumbe hizo, jambo lililosababisha uhasama na kesi za jinai na kijamii.

Mkazi huyo alidai kuwa hatua za usalama zilizochukuliwa na uongozi wa mtaa kama ukaguzi wa magari zilikiuka haki yake ya faragha.Bi Aperera alipewa barua ya malalamishi kuwa alichapisha taarifa za kupaka tope mkazi huyo akidai anashirikiana na wezi.

Baadaye, polisi kutoka kituo cha Lang’ata walimtembelea nyumbani kwake, na afisa mmoja aitwaye George alimwandikia ujumbe wa maandishi akimtaka kufika kituoni kujibu mashtaka.

Hatua hii ilimfanya Aperera kukimbilia Mahakama Kuu ya Kibera, akidai ukiukaji wa haki zake. Aliwashtaki DPP, Inspekta Jenerali wa Polisi na Mkuu Kituo cha Polisi cha Lang’ata.

Katika kesi nyingine ya WhatsApp, Bw Pharis Mukuria alifikishwa kortini Kibera kwa kosa la unyanyasaji wa kimtandao dhidi ya jirani yake.

Alidaiwa kuandika kwenye kundi la WhatsApp la Mwarubaini Court kwamba mwanamke kutoka nyumba fulani anauza dawa za kulevya.

Alipohojiwa, alijitetea na kusema alimaanisha nyumba tofauti, lakini tayari madhara yalikuwa yamefanyika.Alisamehewa na korti ya chini lakini DPP alikata rufaa na Mahakama Kuu ikarejesha kesi.

Jaji Kavedza alisema ushahidi unaonyesha huenda Bw Mukuria alitenda kosa hilo.

Iwapo atapatikana na hatia, anaweza kufungwa hadi miaka 10 au kutozwa faini ya Sh20 milioni au adhabu zote mbili.

Mahakama ilishangazwa na uamuzi wa korti ya chini kuachilia mshtakiwa lakini pia ilipendekeza afikishwe mahakamani kwa kesi ya kijamii.

Katika kesi nyingine Nairobi, Mahakama ya Milimani, Dkt Selina Vukinu alimshtaki jirani yake Godfrey Onyango, wote wakiwa wakazi wa Greenpark Cluster Three, Machakos.

Bw Onyango alitozwa faini ya Sh 2 milioni na Jaji Asneth Ongeri kwa kutumia maneno yasiyochapishika kwenye kundi la WhatsApp la mtaa huo.

Maneno hayo yalihusiana na uamuzi wa Dkt Vukinu kusimamisha ujenzi uwanjani kwa amri ya mahakama hadi kesi fulani isikizwe.

Katika kaunti ya Nakuru, afisa wa shirika la misaada, Bi Sarah Rosborg, aliagizwa kumlipa Bi Anne Marie Tipper Sh2.5 milioni kwa kuchapisha ujumbe wa kukashifu kuhusu fedha za wafadhili katika kundi la WhatsApp la shirika lao “Play Kenya Managers”.

Jaji Samuel Muchochi alisema: “Hakuna ubishi kuwa ujumbe huo ulichapishwa na mshtakiwa kwenye kundi hilo. Hakuthibitisha ukweli wa ujumbe huo, wala hakuwa na sababu halali ya kuuchapisha.”