Utata wazuka kuhusu kilichomuua mbunge
Na SHABAN MAKOKHA
UTATA ulizuka Jumapili kuhusiana na chanzo cha kifo cha Mbunge wa Matungu, Bw Justus Murunga, aliyefariki Jumamosi usiku.
Tangu habari za kifo chake zilipotangazwa, chanzo cha kifo chake kiliibua mdahalo mkali huku baadhi ya viongozi na wananchi wakiamini alikufa kwa ugonjwa wa Covid-19.
Jumapili, familia yake ilisisitiza mwanasiasa huyo aliaga dunia kwa kuugua ugonjwa wa kisukari na mshtuko wa moyo.
Nduguye Mbunge huyo, Bw Henry Washishwa, alisema Bw Murunga alilazwa katika hospitali moja jijini Mombasa mwaka 2019 ambapo iligunduliwa alikuwa akiugua kisukari.
Mnamo Novemba 11, 2020, Bw Murunga alilalamikia maumivu ya kifua na akapelekwa hadi hospitali ya Aga Khan, jijini Kisumu.
Alilazwa hospitalini humo kwa siku nne kisha akaruhusiwa kuenda nyumbani kwake kijiji cha Ebumakunda, Matungu Alhamisi wiki iliyopita.
“Hali yake ya afya ilikuwa thabiti alipoondoka hospitalini na hakuwahi kuwa mgonjwa au kulazwa katika hospitali yoyote ile. Mnamo Novemba 11, 2020, alilalamikia maumivu ya kifua na tukamshauri atafute huduma za kimatibabu,” akasema Bw Washishwa.
Aidha Bw Washishwa ambaye ni meneja wa Hazina ya Fedha za Maendeleo ya Eneobunge hilo (CDF), alifichua kwamba ripoti za kimatibabu zilionyesha nduguye aliaga dunia kutokana na ugonjwa wa kisukari wala si virusi vya corona jinsi inavyodaiwa.
Jumamosi, Bw Murunga aliwakaribisha marafiki waliomtembelea kumtakia afueni nyumbani kwake.
“Alikuwa ametukaribisha nyumbani kwake na alionekana mwenye furaha mno. Tulikuwa na matumaini kwamba alikuwa anaelekea kupona,” akasema Bw Athman Magara.
Baadaye jioni alianguka chini na familia yake pamoja na wasaidizi wake wakamkimbiza hadi hospitali ya kaunti ndogo ya Matungu karibu na nyumbani mwake.
Hata hivyo, walimhamisha hadi hospitali ya St Mary’s Mumias baada ya kukosekana kwa vifaa vya kuwasaidia wagonjwa kupumua katika hospitali ya Matungu.
“Hospitali yetu ingekuwa na vifaa vya kuwasaidia wagonjwa kupumua pengine tungeokoa maisha yake. Hata hivyo, safari ya kutoka Matungu hadi Mumias ilikuwa ndefu na hatukufaulu kumwokoa,” akaongeza Bw Washishwa.
Mdahalo mwingine uliibuka jana wakati ilipofichuka mwili wake ulikuwa unasafirishwa hadi katika hifadhi ya maiti ya Lee jijini Nairobi, ilhali inatarajiwa ataziwa Kakamega.
Mbunge wa Mumias Mashariki, Bw Benjamin Washiali alisema Tume ya Huduma za Bunge (PSC) ndiyo itahusika na maandalizi ya mazishi ya marehemu.
“Hadhi yake kama mbunge inatuamrisha tumpe mazishi ya heshima na hilo ndilo tunawajibikia,” akasema Bw Washiali.
Marehemu Bw Murunga alizaliwa mnamo 1961 na akasomea Shule ya msingi ya Kimilili na ile ya upili ya Kamusinga. Baadaye alisomea uhasibu katika Taasisi ya Mafunzo ya Kaimosi na Taasisi ya Mafunzo ya People mjini Nakuru.
Rais Uhuru Kenyatta, Naibu wake William Ruto, kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi na mwenzake wa ODM Raila Odinga, jana walituma rambirambi zao kwa familia ya mbunge huyo.
Wakazi wa Matungu nao walimwomboleza Bw Murunga wakimtaja kama kiongozi mchapakazi ambaye aliinua sana viwango vya elimu na kukumbatia miradi mingi ya kusaidia jamii katika eneo hilo.