Uuzaji wa ardhi kwa Devki kujenga kiwanda cha chuma Taita Taveta wapingwa
UJENZI wa kiwanda cha chuma cha Sh11 bilioni katika Kaunti ya Taita Taveta uko katika hatari ya kukwama baada ya baadhi ya wanachama wa ranchi ya Mbulia kwenda kortini wakitaka kubatilishwa kwa hati miliki ya ekari 500 zilizopewa kampuni ya Devki Steel Mills Ltd.
Wanachama hao 56 waliwasilisha kesi hiyo katika Mahakama ya Mazingira na Ardhi mjini Voi wakidai kuwa hawakuhusishwa katika shughuli ya kutoa kipande hicho cha ardhi kwa mwekezaji huyo ili kujenga mradi huo.
Wanadai kuwa mchakato huo ulifanywa bila wao kujua wala kutoa maoni yao, hivyo kukiuka haki zao kama wadau katika shamba hilo linalomilikiwa na jamii ya eneo la Ngolia.
Mmoja wa wanachama hao Bw George Mwasighwa aliyeapa kwa niaba ya wenzake 55:Â wanachama hao wanadai kuwa kamati ya ranchi, kwa siri na bila kuwajulisha, iliamua kuiuzia kampuni hiyo ekari 500 za shamba kwa Sh50 milioni.
Anadai kuwa kipande hicho cha ardhi kiliuzwa kwa bei ya chini, jambo ambalo lilikiuka haki yao ya kutoa maoni wakati wa kufanya maamuzi mazito kuhusu ardhi yao.
Bw Mwasighwa alisema kuwa kamati hiyo haikufuata taratibu zilizowekwa wakati wa kukata ardhi ya ranchi hiyo ya ekari 37,000.
Wanachama hao wameshtaki usimamizi wa ranchi hiyo, kampuni ya Devki Steel Mills, msajili wa ardhi ya jamii, serikali ya kaunti na Mwanasheria Mkuu.
Wanaitaka mahakama hiyo kutangaza hatua za kamati hiyo kuwa ni batili na kuamuru msajili wa ardhi kuandaa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa ranchi hiyo ndani ya siku 60 za hukumu.
Vilevile, wanaitaka mahakama itangaze kuwa uamuzi wa kugawa na kuuza ardhi hiyo kwa kampuni ya Devki Steel Mills Ltd ni batili kutokana na kutoshirikishwa kwa wananchi, kinyume na Katiba.
“Vitendo vya ranchi hiyo na dhamira yake vinahitaji kukomeshwa mara moja kwani kuna mipango ya kampuni iliyouziwa kuanzisha mradi mkubwa katika ardhi hiyo,” ombi hilo lilisema.
Bw Mwasighwa alisema kuwa uamuzi wa kamati ya ranchi hiyo ni kinyume na haki ya ushiriki wa umma na vile vile kudai kuwa kamati hiyo imekuwa ikifanya kazi kinyume cha sheria tangu muda wao wa kukaa madarakani umalizike.
Alidai kuwa tangu ingie madarakani mwaka 2021, hakuna mkutano haukupangwa ili kuwapa taarifa wanachama kuhusu masuala ya ranchi hiyo.
“Uamuzi wao wa kuuza ardhi umeegemezwa kwenye msimamo usio halali kwani muda wao wa umiliki ulikuwa wa miaka 3. Jinsi mambo yalivyofanyika mtu anaweza kusoma uovu ndani yake kwani kushughulikiwa kwa hati miliki kulikuwa kwa kasi,” ombi hilo linasema.
Kampuni ya Devki Steel Mills, mdau mkuu katika sekta ya chuma nchini Kenya, inapanga kujenga kiwanda cha chuma kwenye ardhi hiyo iliyonunuliwa.
Hili ni jaribio la pili kwa mwekezaji huyo kujenga kiwanda hicho katika eneo hilo baada ya kushindwa wakati wa utawala uliopita.
Mwekezaji huyo alipanga kuanza ujenzi mwezi huu na kukamilika ndani ya miezi minane.
Katika ziara yake katika kaunti hiyo majuma mawili yaliyopita, Rais William Ruto alisema atarejea huko kuzindua ujenzi wa kiwanda hicho kabla ya mwisho wa mwezi huu.
Mradi huo unatarajiwa kutoa nafasi za kazi kwa zaidi ya watu 3,000 wakati wa ujenzi na zaidi ya watu 2,000 utakapoanza kufanya kazi.