Habari

Uzembe wa Bunge unavyopalilia mtindo wa mahubiri tatanishi nchini

Na DAVID MWERE April 27th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KUKOSA kwa Bunge kupitisha sheria ya kudhibiti mashirika ya kidini kuwalinda Wakenya dhidi ya viongozi wa kidini wanaotoa mafunzo ya kupotosha kumechangia kuwepo kwa makundi ya kidini yenye misimamo mikali.

Makundi haya yanaendelea kufanya shughuli zao ambapo katika kisa cha punde zaidi watu wawili waliripotiwa kufariki katika kanisa moja huko Migori.

Mswada wa Mashirika ya Kidini wa Mwaka 2024, uliotokana na uchunguzi wa Seneti kuhusu mauaji ya Shakahola, ulilenga kudhibiti kuibuka kwa makanisa tata na kuyatoza ushuru kutokana na mapato ya sadaka na zaka.

Hata hivyo, mswada huo haukuchapishwa kutokana na shinikizo kutoka kwa viongozi wa kidini walioupinga.

Mswada huo ulipendekeza faini ya Sh5 milioni au kifungo cha hadi miaka mitatu jela, au adhabu zote mbili kwa wamiliki wa mashirika ya kidini ambayo hayajasajiliwa.

Jumapili, Seneta wa Tana River Danson Mungatana, ambaye alikuwa mwenyekiti wa kamati ya muda ya Seneti iliyochunguza mauaji katika msitu wa Shakahola, alifichua kuwa mswada huo uliondolewa kutokana na malalamishi ya viongozi wa kidini.

Hata hivyo, Seneta wa Makueni Dan Maanzo alipinga mswada huo akisema kuwa Kenya tayari ina sheria za kutosha kushughulikia uhalifu wa aina hiyo.

Kanisa tatanishi la Malkio St Joseph Mission of Messiah in Africa eneo la Opapo, Rongo, Migori. Picha|George Odiwuor

Uchunguzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) ulionyesha kuwa miili hiyo ilikuwa ya wafuasi wa Pasta Paul Mackenzie wa Kanisa la Good News International, aliyewahadaa wafuasi wake wafunge hadi kufa kwa njaa.

Kufikia mwisho wa mwaka jana, zaidi ya miili 400 ilikuwa imetolewa kutoka kwa makaburi ya muda, huku zaidi ya watu 600 wakiendelea kuripotiwa kutoweka.

Licha mauaji hayo serikali inaonekana kutojifunza lolote kutoka Shakahola, kwani wafuasi wawili wa kanisa la Melkio Saint Joseph Missions of Messiah Africa walifariki ndani ya kanisa baada ya kukataa kwenda hospitalini, kutokana na ushawishi wa kidini.

Takribani waumini 57 wa kanisa hilo walikataa kurudi nyumbani wakisisitiza kuwa wangeendelea kukaa katika kanisani licha ya vifo hivyo.

Miili iliyofukuliwa Shakahola ambapo wengi wa waathiriwa walikuwa watoto. Mhubiri Paul Mackenzie amehusishwa na vifo hivyo. Picha|Kevin Odit

Hadi sasa, hakuna mtu aliyeshtakiwa kuhusiana na vifo hivyo, huku hofu ikitanda kuwa shughuli za kanisa hilo zinaweza kufanana na za Shakahola.

Ili kushughulikia ongezeko la mafunzo hatari ya kidini, mswada uliokuwa umependekezwa ulilenga kuanzishwa kwa Ofisi ya Msajili wa Mashirika ya Kidini (ORRO).

ORRO ingesajili na kudhibiti mashirika ya kidini na kuhakikisha yanafuata sheria.uswada huo ulisema:

“Mtu yeyote hataruhusiwa kuanzisha, kuendesha au kusaidia katika kuendesha shirika la kidini bila kusajiliwa kwa mujibu wa sheria hii.”