Habari

Valentino yasisimua wengi kwa njia tofauti

February 14th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na WAANDISHI WETU

SIKUKUU ya Wapendanao almaarufu St Valentino iliadhimishwa Ijumaa ulimwenguni kote ambapo Wakenya walijitokeza kuisherehekea kwa namna mbalimbali licha ya baadhi kulalamikia hali ngumu ya kiuchumi.

Uchunguzi wa haraka uliofanywa na ‘Taifa Leo’ katika maeneo mbalimbali nchini ulionyesha Wakenya wengi wakiendelea na kazi zao kama kawaida ambapo biashara zikifunguliwa mapema.

Hata hivyo, baadhi ya watu walionekana wakiwa wamebeba maua na kuvalia mavazi ya rangi nyekundu inayohusishwa na siku hiyo huku biashara ya maua na zawadi nyinginezo ikivuma mchana kutwa.

Baadhi ya wakazi wa Nairobi na Nakuru waliamua kusherehekea Valentine’s Day kwa namna tofauti kwa kutoa damu.

Katika jiji la Nairobi, wakazi walimiminika katika uwanja wa KICC, ili kusherekea Sikukuu ya Wapendanao kwa kutoa damu kwenye shughuli iliyoandaliwa na shirika la Onyesha Upendo Wako.

“Nilianza kutoa damu nikiwa na umri wa miaka 17, nimetoa damu mara 64. Ninawahimiza Wakenya kujitolea kutoa damu ili kuonyesha upendo wao. Ninawahimiza pia vijana kujitolea kutoa damu mara kwa mara kwa sababu kufanya hivyo kutawawezesha kuwa makini,” alisema Bi Aisha Dafala mwenye umri wa miaka 57.

Katika Kaunti ya Mombasa, wahudumu wa Matatu kwa mara ya kwanza walipata fursa ya kipekee ya kusherehekea Sikukuu ya Wapendanao baada ya kuandaliwa sherehe maalum.

Shirika la Heels and Wheels Africa (HAWAFRICA) pamoja na Mombasa Matatu Gallery (MMG) kwa mara ya kwanza liliwaandalia wahudumu wa matatu hafla maalum ya kuadhimisha Siku ya Wapendanao.

Mamia ya wakazi wa Nakuru pia waliamua kusherehekea Valentino kwa kwa kutoa damu ili kuwasidia wagonjwa katika sehemu mbalimbali nchini.

Hata hivyo, mjini Kakamega, mbwembwe na shamrashamra zinazohusishwa kwa kawaida na sikukuu ya Valentino zilikuwa chache huku wakazi wakilalamikia hali ngumu ya kiuchumi.

Wauzaji maua kama vile Morgan Wafula, walilalamika kwamba ni wapenzi wachache waliojitokeza kununua maua na zawadi nyinginezo.

Wakati huo huo, shirika la Missing Voices liliadhimisha sikukuu ya Valentino kwa kusema kwamba Wakenya 107 wengi wao wakiwa vijana katika vitongoji duni waliuawa na polisi mwaka 2019.

 

Ripoti ya Mary Wangari, Benson Amadala, Phyllis Musasia, Isaac Wale, Farhiya Hussein na Titus Ominde