Vibarua wa Wanjigi kizuizini kwa ‘kuhifadhi’ grunedi nne
KUSAKWA kwa kiongozi wa chama cha Safina Jimi Wanjigi na maafisa wa polisi kwa tuhuma anafadhili maandamano ya Gen Z kuliwachongea wafanyakazi wake.
Vibarua wawili waliokuwa wameajiriwa na mwanasiasa huyo nje ya makazi yake mtaani Muthaiga walidaiwa kuhifadhi na grunedi nne.
Bw Wanjigi amekanusha alihusika na kufadhili maandamano ya Gen Z.
Pia amekana alikuwa na silaha hatari na “kamwe hajui ikiwa polisi walikuta gari imeegeshwa nje ya makazi yake ikiwa na silaha”
Vibarua hao Dancan Odhiambo Otieno na Calvin Ochieng Odongo walizuiliwa hadi Agosti 12,2024.
Wakati huo, hakimu mkuu mahakama ya Milimani Bernard Ochoi ataamua ikiwa wataachiliwa kwa dhamana ama watazuiliwa kwa siku 14 kuhojiwa na kuchunguzwa kuhusu silaha hizo hatari.
Washukiwa hao waliwakilishwa na kwa wakili John Andati mahakamani.
Bw Andati alisema “hakuna namna vibarua wanaweza kuwa na grunedi hizi. Wamewekelewa tu.”
Bw Andati aliomba mahakama iwaachilie kwa dhamana akisema “polisi watakuwa na kibarua kigumu kueleza jinsi silaha zinazopatikana na vyombo vya usalama vinamilikiwa na wananchi wasio na ufahamu wowote wa silaha.”
Hakimu aliombwa aamuru Odongo na Otieno wazuiliwe kwa siku 14.
“Hii mahakama itatathmini kwa undani ombi la viongozi wa mashtaka James Gachoka na Herbert Sonye washukiwa hawa wawili wazuiliwe kwa siku 14 au la polisi kukamilisha uchunguzi na kubaini ukweli kuhusu grunedi nne zilizopatikana ndani ya gari walimokuwa ndani,” Bw Ochoi alisema.
Mabw Gachoka na Sonye waliomba Odongo na Otieno wazuiliwe kwa siku 14 kuhojiwa kuhusu silaha hizo hatari.
Mahakama ilielezwa washukiwa hawa walikamatwa nje ya makazi ya Bw Wanjigi mnamo Agosti 8,2024 na ndani ya gari walimokuwa mlipatikana grunedi nne.
“Twaomba muda silaha hizi zipelekwe kukaguliwa na wataalamu wa silaha kubaini ikiwa zimo katika hali ya kutumika ama muda wake umepita,” Bw Gachoka alimweleza hakimu.
Bw Wanjigi ambaye amekataa katakata amekuwa akifadhili maandamano alisakwa kwa udi na uvumba na polisi usiku kucha Agosti 8,2024 lakini hakuonekana.
Bw Ochoi alifahamishwa Ijumaa Agosti 9,2024 kwamba polisi waliwaandama Wanjigi na msafara wa magari aliokuwa nao katika maandamano hadi mtaani Muthaiga , Nairobi.
Nje ya makazi yake ya kifahari ya Wanjigi polisi waliwakamata Otieno na Odongo na kupata silaha na vifaa vya mawasiliano.
Hakimu alielezwa vibarua hawa wawili walitiwa nguvuni kwa misingi ya kisiasa tu.
Bw Ochoi aliombwa atupilie mbali ombi la kuwazuilia Odongo na Otieno kisha iamuru waachiliwe.