Vifo zaidi huku maporomoko mengine ya ardhi yakikumba Elgeyo Marakwet
WATU wawili zaidi wamethibitishwa kufa katika maporomoko mengine ya ardhi yaliyotokea katika eneo la Kapkenda, Keiyo Kaskazini, kaunti ya Elgeyo Marakwet huku idadi ya waliokufa katika mkasa sawa na huo Marakwet Mashariki ikifika 26.
Wawili hao nyaya mwenye umri wa miaka 57 na mjukuu wake mwenye umri wa miaka 11 walikufa Jumapili (Novemba 2, 2025) usiku huku mvua kubwa ikiendelea kushuhudiwa katika eneo hilo la Bonde la Kerio.
Gavana wa kaunti ya Elgeyo Marakwet Wisley Rotich alithibitisha kuwa kisa hicho kilitokea Jumapili usiku.
“Maafisa wa kukabiliana na majanga katika kaunti, maafisa wa afya, chifu na wakazi walifika katika eneo la tukio na kuwakimbiza waathiriwa katika Hospitali ya Rufaa ya Iten. Lakini inasikitisha kuwa tumewapoteza watu wawili baada ya mwamba mkubwa kugonga nyumba ambamo walikuwa,” akaeleza.
Mzee Joseph Chemweno ambaye aliponea kifo kwa tundu la sindano alielezea kilichotokea.
“Nilisikia sauti ya kiajabu tulipokuwa tukila chajio. Ghafla bin vuu, mke wangu na mjukuwe walikuwa wamefinywa na miamba mikubwa iliyokuwa imeteremka kutoka mlimani. Juhudi za kuwaokoa hazikufua dafu,” akaeleza.