Vijana Lamu wadai kazi za mjengo katika mradi wa nyumba zinatolewa kwa upendeleo
VIJANA wenyeji wa Kaunti ya Lamu wanalia kubaguliwa kwenye nafasi zinazotolewa za ajira ya ujenzi wa nyumba za bei nafuu.
Mradi huo unaendelezwa mjini Mokowe baada ya kufunguliwa rasmi na Rais William Ruto Februari mwaka huu.
Licha ya ahadi, ikiwemo kutoka kwa kiongozi huyo wa taifa kwamba mradi ungefaidi pakubwa vijana wenyeji, imebainika kuwa wengi wa wale wanaofanya kazi za ujenzi Mokowe ni vijana kutoka nje ya Lamu.
Baadhi ya vijana wenyeji waliohojiwa na Taifa Leo walimlaumu mwanakandarasi kwa kuja na vibarua wake tayari kutekeleza kazi kwenye mradi husika.
Omar Ali alishikilia haja ya kutimizwa kwa ahadi ya Rais Ruto kwamba vijana wenyeji wangepewa kipaumbele kuhusiana na nafasi za ajira mradini.
Bw Ali alieleza masikitiko yake kwamba vijana wengi wa Mokowe, Hindi, Lamu na viunga vyake wamesalia kurandaranda mitaani bila ajira licha ya mradi huo mkubwa wa ujenzi kuendelezwa.
“Tulitarajia kupona kiajira punde Rais Ruto alipoanzisha ujenzi wa nyumba za bei nafuu. Tuliahidiwa kwamba mradi utalenga kutupa ajira sisi wenyeji ila mambo si hivyo. Wasimamizi wa mradi walifika na watu wao, hivyo kutunyima ajira. Rais Ruto atusaidie,” akasema Bw Ali.
Kauli yake iliungwa mkomo na Bw Athman Bakari aliyeshinikiza wanaojishughulisha na kazi za ujenzi wa nyumba za bei nafuu mjini Mokowe kukaguliwa na kuhakikiwa iwapo kweli ni wenyeji wa Lamu.
“Twataka uchunguzi wa haraka ufanywe. Wafanyakazi vibarua na wengineo wakaguliwe upya. Ikiwa wewe si makzi wa Lamu utupishe sisi wenyeji ambao hatuna ajira ili pia tufaidike,” akasema Bw Bakari.
Wakati wa uzinduzi wa mradi huo wa ujenzi wa nyumba za bei nafuu mjini Mokowe, viongozi mbalimbali waliozungumzwa wakiongozwa na Gavana Issa Timamy pia walikariri wito wa mradi kufaidi vijana wa eneo hilo.
Bi Karembo Masha, mkazi wa Mokowe, pia aliomba jinsia zote zizingatiwe katika utoaji wa nafasi za ajira kwenye mradi husika.
“Tuliwasikia wabunge, madiwani, seneta na Gavana Timamy wakisisitiza kwamba mradi ufaidi wenyeji. Tunawataka hao viongozi wajitokeze ili watutetee kuhakikisha kazi hizo tunapewa sisi wenyeji. Isitoshe, wanawake pia wazingatiwe katika utoaji wa hizo ajira. Pia twaweza,” akasema Bi Masha.
Eneo la Mokowe lipatikanalo Lamu Magharibi ni makazi ya karibu watu 4000.