Vijana wachoma kituo cha kwanza cha polisi alichozuiliwa Ojwang
VIJANA waliokuwa na hasira waliteketeza kituo cha polisi cha Mawego katika eneo la Rachuonyo Kaskazini wakati wa ibada ya mazishi ya mwalimu aliyeuawa, Albert Ojwang’.
Ojwang’ alifariki dunia akiwa mikononi mwa polisi jijini Nairobi.
Awali, alikuwa amezuiliwa katika kituo cha p;olisi cha Mawego baada ya kukamatwa na polisi nyumbani kwa wazazi wake katika Kijiji cha Kakoth, eneo la Kokwanyo, katika eneobunge jirani la Kabondo Kasipul.
Mipango ilikuwa imewekwa ili ibada ya mazishi ifanyike katika Shule ya Msingi ya Nyawango, ambapo masomo yalisitishwa ili kutoa nafasi kwa umati mkubwa wa waombolezaji.
Mahema yaliandaliwa kwa waombolezaji kutazama mwili.
Hata hivyo, mambo hayakwenda kama ilivyopangwa.
Baada ya mwili kuwasili Lida, gari la kubeba maiti lenye kioo cha wazi kilichowawezesha waombolezaji kuona jeneza lilitarajiwa kuelekea moja kwa moja nyumbani kwa mwendazake.
Lakini vijana waliokuwa wameungana na wanafunzi kutoka Chuo cha Ufundi cha Mawego walifunga barabara na kusisitiza kuwa mwili upelekwe kwanza katika kituo cha polisi cha Mawego.
Baba wa marehemu, Bw Meshack Opiyo, alijaribu kuwaomba waombolezaji waruhusu familia kupeleka mwili moja kwa moja nyumbani.
Yeye, mkewe Eucabeth Adhiambo na mjane wa Ojwang’, Nevnina Onyango, walikuwa kwenye gari moja.
Bw Opiyo alisimama juu ya paa la gari huku akizungumza kwa kipaza sauti kilichounganishwa kwenye mfumo wa sauti uliokuwa kwenye lori lililokuwa sehemu ya msafara wa mazishi.
Lakini hakuna aliyemsikiliza.
Kelele za umati zilikuwa nyingi kiasi kwamba sauti yake haikusikika.
Vijana walijitwika jukumu la kuutoa mwili kutoka kwenye gari la maiti na wakabeba jeneza kwa mikono yao, wakitembea takriban kilomita tatu hadi kituo cha Polisi cha Mawego.
Walipofika kituoni, baadhi yao walianza kurusha mawe wakilenga madirisha. Kufikia wakati huo, maafisa wa polisi waliokuwa kituoni humo walikuwa wamekimbia.
Hakukuwa na yeyote wa kulinda kituo hicho.
Baada ya kugundua kwamba polisi hawakuwepo, vijana walianza kuharibu mali.
Katika vurugu hizo, vijana walishusha bendera mbili – ya Huduma ya Kitaifa ya Polisi na bendera ya taifa.
Kundi moja lilirudisha mwili hadi Soko la Lida na kundi jingine likabaki kituoni kuchoma moto jengo la kituo.
Ofisi ya ripoti iliyojengwa kwa mbao ilishika moto kwa haraka na kuteketea kabisa.
Jengo jingine la kudumu ambalo hutoa makazi kwa maafisa wa polisi pia lilitiwa moto, lakini maafisa wa polisi waliotumwa kutoka vituo mbalimbali waliwasili na kufanikiwa kuuzima.