Habari

Vijana walalamika kukosa kuanza kazi za ‘Climate Worx’ baada ya kuhakikishiwa wako ndani

Na SAMMY KIMATU July 31st, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MPANGO wa kazi kwa vijana unaofahamika kama Climate Worx unakabiliwa na mkanganyiko baadhi ya vijana wakilalama kukosa kuanza kazi kama walivyoahidiwa.

Chini ya mpango huo, vijana huajiriwa kusafisha maeneo ya kandokando ya mito kwa awamu mbili.

Katika eneo la South B, vijana walioajiriwa wiki iliyopita walitarajiwa kuripoti kazini Jumatatu lakini hilo halikutimia.

Kwa mujibu wa duru, machifu na wasaidizi wao wote waliitwa katika makao makuu ya kaunti ndogo ya Kariokor, na hivyo vijana waliokuwa wameitwa hawakuweza kuanza kazi siku hiyo.

“Nilikopa hela nikanunue buti za mvua na koleo baada ya jina langu kuthibitishwa kwenye ofisi ya chifu wa Hazina wikiendi iliyopita. Lakini niliporipoti Jumatatu, chifu aliniambia nisubiri. Sasa ni Jumatano na hakuna taarifa yoyote rasmi kutoka kwa maafisa,” alisema kijana mmoja aliyesononeka.

Akizungumza na Taifa Leo Jumatano, Naibu Kamishna wa Kaunti ya South B Ibrahim Adan, alithibitisha kuwa wiki iliyopita walikamilisha awamu ya kwanza ya kazi kwa vijana.

Bw Adan alisema kuwa jumla ya vijana 500 wataajiriwa na serikali kwa ajili ya awamu ya pili.

Alisema kwamba: katika eneo la Hazina, vijana 150 wataajiriwa, huku Kayaba pia ikipata nafasi za vijana 150.

Katika eneo la Fuata Nyayo, vijana 150 pia wataajiriwa lakini eneo la Landi Mawe litapata nafasi za ajira kwa watu 50 pekee.

Eneo la Landi Mawe lina nafasi chache kwa sababu ya idadi ndogo ya watu, likijumuisha mtaa wa Landi Mawe, Mukuru-Commercial na mitaa ya Kaberira.