Habari

Viongozi Lamu waitaka serikali kuongeza muda wa sensa

August 27th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na KALUME KAZUNGU

VIONGOZI Kaunti ya Lamu wanaishinikiza serikali kuongeza muda wa shughuli inayoendelea ya kuhesabu watu nchini – sensa – ili wakazi walio katika maeneo yanayokumbwa na changamoto za usalama na usafiri eneo hilo wafikiwe.

Shughuli ya kuhesabu watu nchini iling’oa nanga rasmi mnamo Agosti 24 na inatarajiwa kukamilika Agosti 31.

Katika mahojiano na Taifa Leo mjini Lamu, Naibu Gavana Abdulhakim Aboud na Mbunge wa Lamu Mashariki Athman Sharif walisikitika kuwa shughulu hiyo imekuwa ikijikokota katika baadhi ya sehemu za Lamu, ikiwemo Basuba, Milimani, Mangai, Mararani, Kiangwe na Pandanguo – ambazo zote ziko ndani ya msitu wa Boni – na pia Kiunga na Ishakani mpakani mwa Lamu na Somalia.

Maeneo hayo yamekuwa yakishuhudia mashambulizi ya mara kwa mara kutoka kwa al-Shabaab, matukio yaliosukuma serikali ya kitaifa kuzindua operesheni ya Linda Boni ambayo imekuwa ikiendelea tangu mwaka 2015.

Bw Aboud alisema ipo haja ya serikali kurefusha muda wa sensa kwani watu wengi kwenye maeneo hayo hawajafikiwa ili wahesabiwe.

Alisema baadhi ya maeneo pia ni makubwa ilhali idadi yake ya watu ikitapakaa maeneo mbalimbali.

Alisema kipindi cha siku nne zilizosalia kamwe hakitoshi kuwezesha maafisa wa sensa kuwafikia wakazi wote wa Lamu na kuwahesabu.

“Ombi langu kwa serikali ni kwamba iongeze muda wa wakazi hasa wale wa maeneo yenye changamoto ya usalama na usafiri eneo hili kufikiwa na kuhesabiwa. Nimekuwa nikijadiliana na maafisa wa serikali na wakathibitisha kuwa sensa imekuwa ikiendelea kwa kujikokota katika baadhi ya sehemu zetu zenye changamoto. Itakuwa bora kwa serikali kusikia kilio chetu na kuongeza muda wa sensa,” akasema Bw Aboud.

Naye Bw Sharfi alishikilia kuwa lazima serikali ihakikishe watu wote eneo la Lamu wamehesabiwa.

Alisema iwapo mchakato utakamilika huku baadhi ya wakazi wakiwa bado kuhesabiwa, halitakuwa jambo jema.

Haki

Bw Sharif alisisitkiza kuwa suala la changamoto ya usalama eneo la Lamu lisichukuliwe kuwa kigezo cha kuwafanya baadhi ya wananchi kunyimwa haki ya kuhesabiwa.

Alishikilia kuwa ni muhimu kwa idadi ya watu Lamu kubainika kikamilifu ili kuiwezesha serikali kutengea eneo hilo mgao wa fedha unaostahili kila mwaka.

“Lamu imekuwa ikipokea mgao wa chini kabisa wa fedha kutoka kwa serikali kuu kila mwaka ikilinganishwa na kaunti zote 47. Hayo yote yanatokana na kwamba idadi ya watu eneo hili kulingana na sensa ya 2009 ni ndogo mno. Tunahitaji watu wetu wapewe muda wa kutosha ili kujitokeza na kuhesabiwa. Hilo litasaidia Lamu kupata fungu lake linalostahili la fedha ili kuchangia maendeleo eneo hili siku za usoni,” akasema Bw Sharif.

Kauli ya viongozi hao inajiri wakati ambapo idara ya usalama eneo hilo tayari imejitokeza na kuwahakikishia wakazi usalama wao kipindi chote cha sensa na hata baada ya shughuli hiyo kukamilika.

Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Irungu Macharia pia ameahidi kuhakikisha maafisa wa jeshi la Kenya (KDF) wanahusishwa kuhakikisha kuna usalama; hasa kwenye maeneo yanayokumbwa na changamoto za kiusalama Lamu.

Jumatatu, serikali pia ilitangaza kuongeza muda wa kutekeleza sensa kote nchini hasa kwenye sehemu za miji mikuu ambapo watu ni wengi.