Habari

Viongozi walivyotoa misaada ya kuwahonga raia Krismasi

Na WAANDISHI WETU  December 27th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WANASIASA wakuu na maafisa wa serikali wanaomezea mate nyadhifa katika Uchaguzi Mkuu wa 2027 waligeuza sherehe za Krismasi msimu wa kampeni kwa kumwaga mamilioni kupitia misaada ya chakula na kufadhili michuano ya kabumbu.

Yamkini ulikuwa wakati wa kushiriki zawadi za Krismasi lakini kutokana na idadi kubwa iliyoshuhudiwa kupitia picha zilizonaswa na kusambazwa na wanasiasa, ilikuwa ukumbusho wa viwango vya ufukara nchini ambavyo wanasiasa wameendelea kutumia ili kujinufaisha kisiasa.

Katibu wa Wizara ya Afya, Dkt Ouma Oluga na mwenzake wa Kawi, Alex Wachira, ni miongoni mwa maafisa wa serikali waliovamia vijiji kutoa misaada kwa wasiobahatika.

Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki alikaribisha mamia ya majirani zake kusherehekea Sikukuu ya Krismasi makazini mwake Irunduni, Kaunti ya Tharaka-Nithi, ambapo wanawake walipokea zawadi za chakula na wanaume pesa taslimu katika hafla iliyofanyika usiku wa kuamkia Krismasi.

Mnamo Disemba 18, Gavana Susan Kihika na mume wake Sam Mburu waliwakaribisha maelfu ya wakazi makazini mwao, Ngata, ambapo walisambaza bidhaa zikiwemo mafuta ya kupikia, unga wa mahindi, ngano, sukari, mchele, majani chai na sabuni.

Kule Nyandarua, viongozi wanaoegemea mrengo wa Rais William Ruto, Sikukuu ya Krismasi walizunguka kaunti wakisambaza zawadi, kumpigia debe rais huku wakisambaza bidhaa za chakula, nguo na malazi.

Mwakilishi Mwanamke, Faith Gitau na Diwani wa Ndaragwa, Mwangi Kagwe walitumia Krismasi wakisambazia wakazi zawadi.

Mnamo Disemba 17, Gavana wa Kericho, Dkt Erick Mutai, vilevile alikaribisha mamia ya wakazi nyumbani kwake, Chesingoro, ambapo, kulingana na waliohudhuria, alifanya kampeni ya kuwania muhula wa pili.

Seneta wa Vihiga Godffrey Osotsi aliandaa tamasha ya mziki iliyoshirikisha kwaya za madhehebu mbalimbali na kufadhili mashindano ya Mpira wa Kadanda.

Gavana Gladys Wanga naye alisambaza misaada ya chakula usiku wa kuamkia Krismasi ambapo mamia ya wakazi walikusanyika nyumbani kwake Kochia kupokea mifuko ya mchele na maharage.

Siku yenyewe ya Krismasi Mbunge wa Kisumu ya Kati, Joshua Oron aliandaa tamasha zake za kila mwaka za Krismasi zilizovutia mamia ya wakazi na familia za mitaani.

Seneta wa Kisumu, Tom Ojienda, anayemezea mate ugavana, alishiriki Krismasi na wakazi nyumbani kwake Awasi.

Katika Kaunti ya Nyeri, Bw Wachira aliandaa hafla mbili usiku wa kuamkia Krismasi katika eneobunge la Kieni ambapo alisambaza zawadi na kuitisha umoja Mlima Kenya.

Gavana wa Murangá Irungu Kang’ata, Seneta Mteule Veronica Maina na Mbunge wa Gatanga, Edward Muriuki, walijitokeza wakiwa na unga wa mahindi, ngano, mchele na mafuta ya kupikia kwa raia maeneo yao kusherehekea Krismasi.

Bw Kang’ata aliepuka mikutano ya hadhara kwa kutumia teknolojia kusambaza zawadi zake za Krismasi.

Katika Kisii, Gavana Simba Arati alizuru hospitali ambapo aliwapa wagonjwa zawadi.